KIUNGO wa kimataifa wa Yanga Mzimbabwe, Thaban Kamusoko, amefurahishwa na kitendo cha kocha wake, Hans van der Pluijm, kumpa kitambaa cha unahodha kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Kamusoko alivaa kitambaa cha unahodha kwenye mchezo huo ambao mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Yanga walionekana kurejesha makali yao baada ya kuiadhibu Mtibwa Sugar mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kamusoko alisema kuvaa kitambaa cha unahodha na kuiongoza timu kubwa kama Yanga ni heshima kubwa kwake na kuahidi kuendelea kuifanyia makubwa timu hiyo.
“Hiki kitambaa mpaka ukivae unatakiwa ufanye kazi kubwa, hii ni heshima kubwa kwangu kupewa kitambaa hiki,” alisema Kamusoko.

 
Alisema kuwa nahodha wa timu si jambo dogo na kusisitiza wachezaji wote ndani ya kikosi cha Yanga wamejipanga kuhakikisha msimu huu wanatetea taji lao.
“Tunapita katika kipindi kigumu lakini yote ni mipango ya Mungu, hatukuwa na matokeo mazuri katika michezo yetu miwili kila mmoja wetu anatambua hilo tumejipanga kufanya vizuri,” alisema Kamusoko.
Kamusoko alivaa kitambaa hicho baada ya kukosekana kwa mastaa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou na Haruna Niyonzima ambao ndio wamekuwa wakipokezana kitambaa hicho.

Post a Comment

 
Top