SAFARI ya ndege kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza imeonekana kuwaponza wachezaji wa Simba ambao wamewekwa kitimoto kutokana na aina ya mavazi waliyotumia kwenye usafiri huo.
Hatua hiyo ya Simba inakuja baada ya wadau na watani zao wa jadi Yanga kuwacheka wachezaji hao kutokana na aina ya mavazi waliyovaa.
Simba ambao wamepanda ndege baada ya siku 413, mara ya mwisho kutumia usafiri huo wa anga ilikuwa Septemba 8, mwaka jana wakati ikitoka kisiwani Pemba kwenda Tanga kuumana na African Sports katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ilishinda mabao 2-0.
Picha zilizosambaa mitandaoni zinawaonyesha baadhi ya wachezaji wa Simba wakiwa wamevaa yebo za rangi tofautitofauti zikiwemo za njano
Meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, alisema mara baada ya kufika mkoani Shinyanga amelazimika kukaa chini na nyota hao kuwapa darasa.


“Jana asubuhi nimekaa nao wachezaji na nimezungumza nao sidhani kama itajitokeza tena, mambo mengi nimeongea nao ikiwemo suala nzima lililojitokeza la aina ya mavazi,” alisema.
Akizungumzia maendeleo ya mshambuliaji wao, Fredrick Blagnon, aliyeumia kwenye mchezo dhidi ya Toto Africans, alisema wamemwacha Dar es Salaam kutokana na kuwa hali yake bado haimruhusu kutumikia timu hiyo kwa sasa.
“Blagnon amebaki Dar na kama mnavyojua anapaswa kukaa nje ya uwanja kwa wiki moja hivyo tumeshauriwa apumzike,” alisema

Post a Comment

 
Top