WAKATI Simba ikiingia kwenye maandalizi ya mchezo
wao mgumu unaofuata dhidi ya Prisons, italazimika kuikosa huduma ya kocha wake
msaidizi, Mganda, Jackson Mayanja ambaye jana alitarajia kurejea kwao, Kampala.
Mayanja ambaye amesaidiana na bosi wake,
Mcameroon, Joseph Omog kuiongoza Simba kushinda michezo mitano na kusuluhu
miwili, ikiwa kileleni kwa pointi 17, amekwenda kwao kutokana na matatizo ya
kifamilia.
Mayanja amesema kuwa, atakosekana katika siku za
mwanzoni mwa maandalizi ya mechi na Prisons kwa ajili ya kwenda kutoa pole na
kuzungumza na familia yake baada ya kufiwa na mdogo wake, Ronald Galabuzi.
Simba imepangwa kucheza na Prisons, Oktoba 8,
halafu Oktoba 12 itavaana na Mbeya City.
“Timu kwa sasa imepumzika mpaka Jumanne (kesho)
kwa hiyo naona huu ndiyo muda sahihi na mimi niende japo nyumbani kidogo maana
sikwenda wakati wa msiba, kwa hiyo bora niende nikatoe hata pole, nizungumze na
familia kidogo.
“Msiba huu ndiyo ule uliotokea kama wiki mbili
zilizopita. Sitakaa sana najua kuna mchezo mbele dhidi ya Prisons na Mbeya
City, kwa hiyo itachukua kama siku mbili au tatu kisha nitarejea hapa kuendelea
na majukumu ya timu,” alisema Mayanja.
Post a Comment