Hali hiyo imejitokeza mara baada ya Yanga kupoteza mchezo dhidi ya Stand United, waliofungwa bao 1-0 wakiwa ugenini Uwanja wa CCM Kambarage, mkoani Shinyanga, kabla ya kuja kupata sare ya 1-1 na watani zao, Simba Oktoba mosi, mwaka huu, uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa sasa inadaiwa kuwa muda wowote jipu linaloonekana kuanza kuiva litapasuka, huku kukiwa na taarifa za kutaka kutimuliwa kwa kocha msaidizi, Juma Mwambusi, anayedaiwa kushindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya kumshauri kocha Hans van der Pluijm.
Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Yanga zinadai kuwa kumekuwa hakuna maelewano mazuri baina ya Mwambusi na Pluijm, jambo linalochangia kufanya vibaya kwa timu hiyo.
Imeelezwa kuwa Mwambusi kwa sasa anaonekana kuwa msaada mkubwa kwa wachezaji katika kuwaelewesha juu ya anachokitaka Pluijm kutokana na wengi wao kutoielewe lugha anayoitumia kocha huyo, lakini Mwambusi anashindwa kutimiza majukumu hayo.
Mbali na hilo, imeelezwa kuwa hata pale inapocheza Yanga, Mwambusi amekuwa mgumu kumshauri Pluijm kufanya mabadiliko yanayostahili kulingana na mapungufu yaliyoonekana kwenye mchezo.
Habari hizo zimeeleza kuwa, kutokana na hali hiyo, tayari kuna harakati zimeanza kufanyika kuhakikisha Mwambusi anaondolewa Yanga kumpisha Charles Boniface Mkwassa, huku Pluijm akitarajiwa kupewa majukumu ya Ukurugenzi wa Ufundi pindi akija kocha mpya wakati wa mzunguko wa pili wa VPL.
“Tayari kuna matabaka ndani ya Yanga, hususan katika uongozi, kwani kuna baadhi ya watu wanamtengenezea ‘zengwe’ Mwambusi kuhakikisha anaondoka ndani ya Yanga, hii inatokana na Pluijm kutofautiana na Mwambusi mara kwa mara, akimtuhumu kutokutoa maelezo sahihi kwa wachezaji.
“Na tayari Mwambusi ameonekana kugundua kinachoendelea ndani ya timu, hivyo wiki iliyopita aliamua kurejea nyumbani kwao Mbeya kwa matatizo ya ya kifamilia, ingawa inasemekana jambo hilo halina ukweli,” alisema mtoa habari wetu.
BINGWA lilimtafuta kocha huyo mbaye aliwahi kuipa mafanikio timu ya Mbeya City kabla ya kutua Yanga, ambapo alikiri kutokuwa na Wanajangwani kwa muda mfupi kutokana na matatizo ya kifamilia yaliyomlazimu kwenda mkoani Mbeya.
Kuhusu suala la kutokuwa na maelewano na Pluijm, Mwambusi alisema jambo hilo halipo na kama linasemwa litakuwa linatengenezwa.
“Kweli sikuwa na timu kwa kipindi kifupi kilichopita kutokana na mambo yangu binafsi yaliyonilazimu kwenda Mbeya, lakini kwa sasa nimesharejea Dar es Salaam, suala la mimi kutokuwa na maelewano mazuri na Pluijm si kweli na iwapo linazungumzwa hivyo basi litakuwa linatengenezwa kwa manufaa ya wazungumzaji,” alisema Mwambusi.
Mwambusi alijiunga na kikosi cha Yanga akiwa msaidizi wa Pluijm, Oktoba mwaka jana, kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu, akiletwa kuziba nafasi ya Mkwasa, aliyepewa jukumu la kuinoa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Post a Comment