BEKI Janvier Bokungu, anayecheza namba mbili katika kikosi cha Simba, amefuta rasmi jina la Hassan Ramadhani ‘Kessy’ kwenye vichwa vya mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi hao.

Kessy alikuwa ni mchezaji tegemeo mno katika kikosi cha Simba, akionekana kuziba vilivyo pengo la watangulizi wake kama Shomari Kapombe, Miraji Adam na Nassoro Chollo.

Baada ya Kessy kutimkia Yanga, akifanya hivyo kwa nyodo, mashabiki wa Simba walionekana kuweweseka kwa hofu ya kukosa mbadala wake.
Hivyo, Wekundu wa Msimbazi hao walianza kutangaza kupinga usajili wa beki huyo wa kulia katika kikosi cha watani wao hao wa jadi, kwani alielezwa kusaini mkataba wakati akiwa bado ni mali yao.

Hapo ndipo matukio kadha wa kadha juu ya sakata la mchezaji huyo yalipofuata, ikiwamo kumkatia rufaa kwa Kamati ya Usajili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katika hilo la usajili, Wekundu wa Msimbazi hao ‘waliangukia pua’, wakiambiwa kuwa mashtaka yao ni ya kimadai zaidi na hayawezi kumzuia Kessy kusajiliwa na timu yoyote.

Wakati sakata la Kessy likiendelea, Simba ilikuwa ikifanya usajili na kufanikiwa kunasa wachezaji kadhaa wa kuziba pengo la beki huyo wa kulia, wakiwamo Bokungu na Malika Ndeule na Hamad Juma.

Kati yao, Bokungu ameonekana kukata kiu ya wapenzi wa Simba ambao pole pole wameanza kumsahahu kabisa Kessy na kwamba dalili zinaonyesha kutokuwa na muda wa kuendelea kufuatilia sakata lake.

Hilo linatokana na ukweli kwamba, Mkongomani ameonyesha kiwango kizuri kwenye michezo mbalimbali ya Simba iliyopita, ukiwamo ule dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.

Bokungu mbali na uwezo wa hali ya juu aliouonyesha katika kukaba, ni mrefu kiasi cha kumwezesha kucheza mipira ya juu kwa ufanisi mkubwa kama ilivyo katika kupandisha timu pale ilipohitajika.


Zaidi ya hayo, Bokungu ameonekana kuwa makini mno anapokabiliana na washambuliaji wa timu pinzani, ikiwamo kusaidia ulinzi wa kati pale mabeki wa kati walipopanda kusaidia mashambulizi au vinginevyo.

Na sasa beki huyo tayari ameingia katika vichwa vya wapenzi wa Simba, akichukuliwa kama mmoja wa wachezaji muhimu ndani ya kikosi cha Wekundu hao, akiwa amewapiga kumbo wenzake wanaogombania nafasi hiyo, Ndeule na Juma ambao wote wamejikuta wakikosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Kocha Mkuu, Joseph Omog.

Post a Comment

 
Top