Straika Mtanzania atoa siri za kocha mpya Yanga
HARAKATI za Yanga kutaka kumleta Jangwani kocha wa Zesco United, George Lwandamina, zinaonekana kuitikisa klabu hiyo na Zambia nzima kuwatokana na ubora wa mwalimu huyo.
BINGWA Jumamosi lilikuwa gazeti la kwanza nchini kuandika taarifa za Lwandamina kusakwa na Yanga, taarifa ambazo kocha huyo mwenyewe alizithibitisha kwa kukiri kuwa amepokea ofa kutoka kwa miamba hiyo ya Jangwani.
Gazeti hili lina taarifa kuwa ofa ya Yanga kwa Lwandamina imeitikisa Zesco, ambapo sasa inadaiwa kuwa mabosi wa klabu hiyo wameanza kuhaha kumbakiza kocha huyo aliyeifikisha timu yao nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kutoa dozi za hatari kwa timu za Kiarabu, ikiwemo Al Ahly ya Misri.
Taarifa kutoka Zambia zinadai kuwa mabosi wa Zesco wanataka kumfunga kocha huyo na mkataba mpya, hasa katika kipindi hiki ambacho mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kufika tamati Februari, mwakani.
Kinachowatisha zaidi mabosi wa Zesco ni hofu kuwa kocha huyo atabomoa kikosi kwa kuondoka na baadhi ya wachezaji muhimu wa timu hiyo, wakiwemo Wakenya, straika Jesse Jackson Were na beki wa kati, David ‘Calabar’ Owino, aliowasajili wakati alipopewa mikoba ya timu hiyo.
Blog hii ina taarifa kuwa katika ofa ya Yanga kwa Lwandamina, ametakiwa kuja na mafundi wawili kutoka Zesco ili kuimarisha kikosi cha miamba hiyo ya Jangwani ambayo imepania kufika mbali zaidi kimataifa msimu ujao.
Taarifa hizo ndizo zimekuwa zikiwalaza macho wadau na mashabiki wa Zesco, ambao hawataki kabisa kusikia Lwandamina na wachezaji hao wakiondoka kwenye klabu hiyo kwa sababu ya mafanikio waliyoyapata kwenye michuano ya Afrika katika msimu huu unaoishia.
Katika hatua nyingine, straika Mtanzania, Juma Luizio ‘Ndanda’, anayecheza soka la kulipwa nchini Zambia katika klabu ya Zesco United, amesema kama Yanga wakifanikiwa kumnasa Lwandamina, basi watakuwa wamelamba dume.
Luizio alisema Kocha Lwandamina ni mzuri sana, lakini kama Yanga wanahitaji kuona matunda yake ni lazima wachezaji wa timu hiyo wawe na nidhamu ya hali ya juu.
“Kama Yanga watafanikiwa kumnasa (Lwandamina), watakuwa wamelamba dume, kwani ni mmoja kati ya makocha wenye msimamo na wasiopenda kuingiliwa majukumu yao, hivyo ili afanye kazi nzuri hawana budi kufuata atakayoyataka,” alisema Luizio.
Yanga wamepanga kumchukua kocha ambaye ana historia nzuri ya kutoa vipigo, hasa kwa timu za Waarabu, akiwa na rekodi ya kucheza hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu, ikivuka kwenye kundi A lililokuwa na timu ngumu kama Al Ahly ya Misri, Wydad Casablanca ya Morocco na Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Katika kundi hilo, walimaliza wakiwa na pointi tisa na kushika nafasi ya pili nyuma ya timu ya Wydad Casablanca ya Morocco, wakizipiga kumbo Al Ahly, ambayo mara kadhaa imekuwa ikiisumbua Yanga.
CHANZO: BINGWA
Post a Comment