WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wamesema wameziba mianya yote ya hujuma kuelekea kwenye mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Mwadui utakaofanyika Uwanja wa Kambarage.
Simba inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza michezo 11 huku wakifuatiwa na mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 24, timu zote zikiwa na idadi sawa ya mechi.
Meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, amesema maandalizi kuelekea mchezo huo yanakwenda vema ikiwa sambamba na kufunga milango yote ya hujuma.
“Tumejiandaa vema kuelekea mchezo huu hasa kwenye suala nzima la hujuma ndio maana mipango yetu hatuwezi kuweka wazi kukwepa mambo hayo,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu programu zao za mazoezi mkoani humo, Mgosi alisema wanajifua vyema huku wakiwa katika hali ya tahadhari kubwa kambini kwao kwa kutoruhusu watu wasiowaelewa kufika kuzungumza na wachezaji.
“Tunahitaji ushindi, tumejipanga vyema na kikosi kiko vizuri sana, suala la kufahamu ni kwamba tumejizatiti kukabiliana na fitina za nje ya uwanja na tunaamini tutapata ushindi,” alisema.
Timu hiyo ambayo ilitua Shinyanga kwa ndege, ilijificha katika Chuo cha Ualimu Shaikom ambako walikuwa wakifanya mazoezi lakini meneja huyo aligoma kutaja hoteli waliyofikia.
Simba ndio vinara wa VPL hadi sasa wakiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 11 huku wakiwa hawajapoteza mechi hata moja. Wapinzani wao Mwadui wako katika nafasi ya 10 wakiwa na pointi 13 walizopata katika mechi zao 11 walizocheza.

Post a Comment

 
Top