AMA kweli mashabiki wa Yanga wanampenda sana kocha wa zamani wa timu yao ambaye kwa sasa anainoa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ Charles Boniface Mkwasa na wamedhihirisha hilo majuzi baada ya kumtaka arudi kuifundisha timu yao.
Mkwasa, ambaye kwa sasa anainoa timu ya Taifa, hivi karibuni alikuwepo uwanjani wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga na Azam FC, ambapo mashabiki wa Wanajangani hao walimvaa na kumtaka arejee kuinoa timu yake hiyo ya zamani.
Hiyo ilitokea baada ya mashabiki hao kuonekana kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo kwa sasa, ikiwa ni pamoja na benchi la ufundi la timu hiyo.
Yanga hadi sasa imecheza mechi nane na kushinda nne, sare tatu na kufungwa mchezo mmoja, huku ikijikusanyia pointi 15, ikiwa imeachwa mbali na wapinzani wao, Simba, wanaoongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 23 na michezo tisa waliyocheza, wakishinda saba na kutoka sare miwili na hakuna mchezo waliopoteza hadi sasa.
Kutokana na hali hiyo, mashabiki wa Yanga wanaonekana kutoridhishwa na kiwango cha timu yao, hali iliyowafanya kumvaa kocha huyo wakati wa mechi yao na Azam, iliyomalizika kwa sare ya bila kufungana na kumtaka arudi Jangwani.

Mkwasa alilazimika kuwatuliza mashabiki hao kwa kuwajibu kuwa yeye yupo tayari kurudi Yanga, lakini kwa sasa ni mwajiriwa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivyo mkataba wake haumruhusu kuondoka, labda iwapo Yanga watamhitaji wafanye mawasiliano na mwajiri wake.
“Mimi nipo tayari kurejea Yanga na kama watanihitaji wanatakiwa kuzungumza na mwajiri wangu ambaye ni TFF, kwani bado nina mkataba nao,” alisema Mkwasa, wakati akiwatuliza mashabiki hao.
Mkwasa aliondoka Yanga Oktoba mwaka jana na kupewa jukumu la kuinoa Taifa Stars, huku nafasi yake Yanga ikichukuliwa na aliyekuwa kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi.

Post a Comment

 
Top