CHAMA cha Wataalamu wa Tiba na Michezo Tanzania (Tasma) kimeandika barua ya malalamiko kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufuatia mmoja wa madaktari wa chama hicho, Richard Yomba kupigwa na Makamu wa Rais wa Simba, Godfrey  Nyange ‘Kaburu’ akiwa na baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni ‘makomadoo’ wa timu hiyo.
 Tukio la kupigwa kwa Yomba lilitokea wikiendi iliyopita kwenye mchezo wa Yanga na Simba uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 uliopigwa Uwanja wa Taifa kufuatia makomandoo wa timu hiyo wakiongozwa na Kaburu kumshutumu daktari huyo kutumika na Yanga  kwa kupulizia dawa katika vyumba vyao ‘dressing room’ kabla ya mchezo huo.


Katibu Mkuu wa Tasma, Nassor Matuzya, amesema wamesikitishwa na kitendo cha udhalilishaji alichofanyiwa daktari mwenzao dhidi ya makomandoo hao wakiwa na kiongozi huyo ambapo tayari wameshaandika barua kwa TFF kuhusiana na tukio hilo.

“Kiukweli kwanza sisi kama chama tumesikitishwa na kitendo kilichofanywa na watu wa Simba kwa kumpiga mtumishi wetu lakini tulimpa ushauri baada ya tukio nini cha kufanya kwa sababu pale tayari kulishakuwa na makosa ya jinai ambayo lazima serikali kwa upande wa sheria ichukue mkondo wake.

 “Pia tumeshatuma malalamiko yetu TFF kuhusiana na suala hilo ambalo siku ile tulimueleza mechi kamishna wa mchezo.

“Licha ya hivyo tutaendelea kufuatilia kuona nini kitakachoamuliwa kwa sababu pia tumeishauri TFF tusajili chama chetu kiweze kujitegemea na tufanye kazi zetu kwa uhuru maana kama kikishindikana basi huenda tukashindwa kwa kuhofia usalama wetu wakati wa kutimiza majukumu yetu,” alisema Matuzya.

Championi Ijumaa lilimtafuta daktari huyo ambaye pia aliwahi kuwa daktari wa Taifa Stars ambapo alifunguka: “Kiukweli kwa sasa siwezi kuongelea suala hilo kwa sababu kesi ipo katika Kituo cha Polisi Chang’ombe kwa ajili ya hatua zaidi.”


Post a Comment

 
Top