KAMA ulidhani mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’ anatania anaposema anataka kuweka hisa ya asilimia 51 katika Klabu ya Simba, utakuwa unakosea, kwani ameanza kufanya mambo makubwa kimyakimya.
Na kwa kuanzia, bilionea huyo ameitisha faili la mikataba ya wafanyakazi wa klabu hiyo, ikiwemo benchi la ufundi pamoja na wachezaji na hii yote ikisemekana ni kutaka kujipanga mapema.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa, mfanyabiashara huyo anataka kujua mishahara wanayolipwa wafanyakazi wote kwa ujumla, jambo ambalo viongozi wa Kamati ya Utendaji wanalitekeleza mapema iwezekanayo.
Simba kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kumkabidhi Mo timu, akiweka hisa hiyo ya asilimia 51, ambapo waliunda kamati ya kupitia katiba yao ili kuongeza baadhi ya vipengele vitakavyowaruhusu kukubali mabadiliko hayo.
Kigogo mmoja ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, tangu mchakato huo kuanza, Mo amekuwa akisaidia kutoa fedha kusaidia mambo mbalimbali, ikiwamo mishahara ya wachezaji kama mwanachama wa kawaida.
“Kwa sasa MO anaisaidia Simba kama mwanachama wa klabu hiyo mwenye mapenzi mema, amekuwa akishirikiana na uongozi katika kulipa mishahara ya wachezaji,” alisema kigogo huyo.
Mbali na mishahara hiyo, pia taarifa kutoka ndani zinadai kuwa bilionea huyo ameagiza basi la kisasa ambalo litawasili muda wowote kwa ajili ya matumizi ya timu na kwamba anataka Simba iwe moja ya timu kubwa Barani Afrika.
Wakati huo huo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema agizo lililotolewa na Serikali kuhusu mfumo wanaoutaka lisiwalaze macho mashabiki wao, kwani wanaendelea kufuata taratibu ipasavyo.
“Serikali haikatai mabadiliko, imetoa agizo kuwa michakato hii ifuate taratibu na ndicho ambacho sisi tunakifanya, niwaambie tu wanachama wetu kuwa viongozi wao ni waumini wa kufuata katiba,” alisema.
Alisema mapema watatoa taarifa rasmi namna mchakato huu utakavyofanikiwa kwa kuzingatia katiba ya Simba, katiba ya nchi na kanuni na sheria zinazosimamia mpira wa miguu.
Post a Comment