PEP GUARDIOLA ametupiwa lawama kutokana na kumdhalilisha kiungo, Yaya Toure (pichani juu) kwa kumuacha nje ya kikosi cha Manchester City kitakachocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi, kwa mujibu wa wakala wa mchezaji huyo.
Kiungo huyo wa Ivory Coast mwenye umr wa maika 33-aliachwa katika hatua hiyo Ijumaa iliyopita bila ya kupewa taarifa na Kocha, Guardiola.
Hata hivyo, Yaya hajakitumikia kikosi cha City katika Ligi Kuu baada ya michezo mitatu chini ya kocha huyo mpya.
Na pigo lingine, kiungo huyo wa zamani wa Barcelona ambaye amebakisha msimu mmoja katika mkataba wake na City - sasa anapaswa kukubali kutokuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza katika Kundi C dhidi ya Barcelona, Borussia Monchengladbach na Celtic ambayo anaichezea kaka wa Toure, Kolo.

Wakala wa Toure, Dimitri Seluk, amelalamika kwamba shinikizo kubwa sasa ni Guardiola kushinda lakini alisisitiza mteja wake atauangalia msimu wote huu akiwa nje ya Uwanja wa Etihad.  
Seluk alisema: “Ni uamuzi wa Pep na tunapaswa kuheshimu hilo.
 “Kama atashinda Ligi ya Mabingwa akiwa na City msimu huu nitasafiri hadi England na nitazungumza kwenye runinga kwamba Pep Guardiola ni kocha bora duniani.
“Lakini kama City haitashinda Ligi ya Mabingwa ninatarajia kwamba Pep atakuwa na jukumu la kumuomba msamaha Yaya Toure kwa kusema kwamba alikosea kumdhalilisha mchezaji mkubwa kama Yaya.

“ Lakini ninachotaka kuwambia ni kwamba Yaya atamaliza msimu wake akiwa na City. Hataondoka katika dirisha la usajili la Januari. Anatarajia kwamba atapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake.”
 Toure na kipa mpya wa Man City, Claudio Bravo aliyenunuliwa kwa dau la Pauni 17 milioni kutoka Barcelona ndio wachezaji pekee katika kikosi cha City ambao wameonja utamu wa kubeba taji la ubingwa wa Ulaya.
Toure alikuwa katika kikosi cha Barcelona kilichoichapa Manchester United 2-0 jijini Rome mwaka 2009.
Hata hivyo, mwaka 2010 Guardiola alimuuza Toure kwa dau la Pauni 24 milioni kwenda Manchester City na ujio wake City ulitabiriwa ungehitimisha maisha ya soka ya staa huyo.
Toure alikataa ofa za kutoka klabu mbalimbali za China ambazo zingemuongeza mshahara mkubwa kuliko ule anaolipwa na City kwa sasa, lakini pia alikuwa anahusishwa kuungana na kocha wake wa zamani wa City, Roberto Mancini katika kikosi cha Inter Milan.
Hata hivyo, baada ya mazungumzo ya kina na Guardiola kocha huyo alimuomba abaki kikosini hapo kwa miezi 12 iliyobaki ili amsaidie kuzoea mazingira ya klabu hiyo pamoja na soka la England kwa ujumla, lakini sasa amemuacha katika kikosi cha Ulaya.
Inaeleweka kuwa Guardiola na benchi lake la ufundi walikuwa wanaumiza kichwa mchezaji wa kumuacha katika orodha hiyo kati ya Toure na beki wa kimataifa wa kimataifa wa Ubelgiji, Vincent Kompany, ambaye alikuwa majeruhi wa muda mrefu.
Hata hivyo, Kompany amefanikiwa kucheza mechi moja ya kirafiki kwa ajili ya kupima afya yake na anaweza kurejea uwanjani muda wowote kuanzia sasa, kitu ambacho kimemfanya Guardiola alikate jina rasmi la Toure katika orodha ya wachezaji 21 waliopelekwa Uefa.
Orodha kamili ya kikosi cha City ambacho imepelekwa Uefa ni Claudio Bravo, Willy Caballero; Bacary Sagna, Vincent Kompany, Pablo Zabaleta, Aleksandar Kolarov, Gael Clichy, John Stones, Nicolas Otamendi; Fernando, Raheem Sterling, Ilkay Gundogan, Jesus Navas, Kevin De Bruyne, Fabian Delph, Leroy Sane, David Silva, Fernandinho; Nolito, Sergio Aguero, Kelechi Iheanacho.

Post a Comment

 
Top