Siku moja tu baada ya Mwenyekiti wa
klabu hiyo, Yusuf Manji, kutoa eneo la ekari 712 za ujenzi wa uwanja na vitega
uchumi vingine vya klabu hiyo eneo la Kigamboni, imeelezwa kuwa mabilionea
wawili wako kwenye mipango mizito ya kuwekeza katika klabu hiyo.
Chanzo cha habari cha gazeti hili
kimeeleza kuwa hata hatua ya Manji kutoa eneo hilo kumetokana na uhakika mkubwa
wa hali ya uwekezaji kufuatia kikao kilichoendeshwa kuhusiana na masuala ya
udhamini na uwekezaji wa klabu hiyo karibuni.
Mabilionea wa makampuni makubwa
nchini, wapo katika mikakati kabambe ya kutaka kuidhamini Yanga na wengine
kufanya uwekezaji kwenye klabu hiyo ya Jangwani ambapo kufuatia kikao kizito
kilichofanyika kwenye Hoteli ya Double Tree, Dar es Salaam hivi karibuni
thamani ya uwekezaji imepanda kwa klabu hiyo.
Miongoni mwa mabilionea waliotajwa
kutaka kuwekeza Yanga ni pamoja na bilionea, Mustapha Sabodo ambaye licha ya
kuwa na mapenzi makubwa na klabu ya Simba, lakini ilielezwa kwamba alivutiwa na
mikakati ya uwekezaji wa kibiashara wa klabu ya Yanga na kwamba alikuwa tayari
kuwekeza Sh bilioni 65 kwenye klabu hiyo.
Wengine ni pamoja na Aliko Dangote
ambaye ametajwa kutaka kuwekeza bilioni 50 huku matajiri wengine wakiendelea
kutafakari kiwango cha dau la kuwekeza na wengine wakitaka kutoa udhamini tu
kwa klabu hiyo.
BINGWA lilimtafuta Sabodo ili
kufahamu ukweli wa taarifa za yeye kutaka kuwekeza katika klabu hiyo mahasimu
na klabu anayoipenda ya Simba ambapo alieleza kuwa suala la uwekezaji wa
kibiashara ni zuri hasa kama lina faida ingawa kwa sasa hajafikiria kuwekeza
kwenye mpira.
“Kuwekeza ni jambo jema hasa kama
linalipa, najua huenda Yanga wana mikakati ya kuvutia sana, lakini kwangu mimi
sijafikiria kuwekeza kwenye mpira,” alisema.
Alisema hakuna tatizo lolote kama
atawekeza Yanga licha ya kwamba yeye ni shabiki wa Simba, kwani biashara
haziingiliani lakini kwa umri wake anahitaji kupumzika kwa kuwa anaamini kuwekeza
kwenye mpira kutamwangaisha sana.
“Napenda mpira na naipenda sana
Simba, tena naiombea ishinde ili nifarijike zaidi. Mpira wa Tanzania unakua na
unavutia sana kuwekeza lakini kwangu mimi hapana, nina mradi mwingine wa sanaa
na michezo ambao nitaufanikisha Dodoma, nadhani huo utatosha kuwa mchango wangu
kwenye sekta ya michezo hapa nchini,” alisema Sabodo.
Yanga ipo katika mkakati wa
kujiendesha kibiashara ili kuondokana na mfumo wa sasa ambao unaifanya klabu
hiyo kutegemea mtu mmoja katika kujiendesha.
Huu ni mkakati ambao utaifanya Yanga
kujiendesha kibiashara na kuondokana na mfumo wa sasa wa kutegemea misaada ya
wafadhili na viingilio vya mlangoni ambavyo vimeshuka kutokana na mechi za ligi
kuu kuonyeshwa katika televisheni.
CHANZO: BINGWA
Post a Comment