Simba yamdai Mavugo
STRAIKA wa Simba Mrundi, Laudit Mavugo, ana deni kubwa sana kwenye klabu yake na tayari miamba hiyo ya Msimbazi imeanza kumkumbusha kuwa hadi kufikia mwisho wa msimu huu kuna kitu anatakiwa kuwa amekilipa kwa mashabiki na wanachama wa mabingwa hao wa kihistoria wa Kombe la Kagame.
Kama Waswahili wasemavyo ahadi ni deni, tayari Meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, amemkumbusha Mavugo kuwa wakati alipotua nchini akitokea Vital’O ya Burundi aliahidi kufunga mabao 30 msimu huu, hivyo anatakiwa kutimiza ahadi yake hiyo kwa Wanamsimbazi.
Mgosi ametoa kauli hiyo baada ya Mavugo kukosa mabao ya wazi kadhaa katika mchezo wao wa juzi dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba walishinda kwa mabao 2-1 na kumtaka kujitathmini kwanza kama anataka kutimiza ahadi yake ya mabao 30 kwa msimu.
Licha ya kufunga bao moja katika mchezo huo ambalo ni la pili kwake katika mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, lakini staa huyo alipoteza nafasi kadhaa za wazi za kucheka na nyavu.
Mavugo alikosa mabao hayo ambayo yangeweza kuipa ushindi mnono zaidi Simba katika dakika ya 26, 29 na 36 kutokana na kukosa umakini pale aliposhindwa kuzitumia pasi mbili za Ibrahim Ajib na moja ya Said Ndemla.
Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Mgosi alitumia muda huo baada ya mechi ya jana kumkumbusha staa huyo kuwa anatakiwa kuwa makini sana kama anataka kutimiza ahadi yake ya kufunga mabao 30 kwa msimu.
Amesema licha ya timu yake kucheza vizuri na kupata ushindi katika mchezo huo, lakini ana imani kama Mavugo angetulia angeweza kuipa ushindi mnono zaidi Simba.
“Tumecheza vizuri, tulistahili kupata ushindi wa zaidi ya mabao manne,” alisema Mgosi: “Kama Mavugo na washambuliaji wengine wangetulia tungeweza kupata ushindi mkubwa zaidi.”
Wakati akisaini mkataba wa kujiunga na Simba, Mavugo alikaririwa akisema kuwa atafunga zaidi ya mabao 30 katika msimu huu wa Ligi Kuu ili kuwapa zawadi mashabiki wa Simba ambao wamemsubiri kwa misimu miwili.
Katika hatua nyingine: Mgosi alisema kikosi cha miamba hiyo ya Msimbazi kilicheza soka la hali ya juu kwenye pambano la juzi dhidi ya Ruvu Shooting huku wachezaji wakielewana sana kitu ambacho kinathibitisha kuwa kocha Joseph Omog amefanyia kazi mapungufu yaliyoonekana katika michezo iliyopita.



Post a Comment