WAKATI zikiwa zimebaki siku nne pekee kabla ya
mechi ya watani Simba na Yanga kupigwa, mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Laudit
Mavugo, ameweka bayana yeye hatachonga sana kuhusu mchezo huo utakavyokuwa,
bali anaelekeza akili na makali yake uwanjani.
Mavugo aliyeifungia Simba mabao matatu mpaka
sasa, kwa mara ya kwanza anatarajia kuiongoza timu yake hiyo kuvaana na Yanga
katika mchezo wa ‘derby’ ya Dar utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Oktoba Mosi, mwaka
huu.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Vital’O ya
Burundi, amesema licha ya presha ya mchezo huo inavyozidi kupanda lakini kwa upande
wake hataki kuzungumzia lolote kuhusiana na wapinzani wao, bali atawaonyesha
watakapokutana uwanjani.
“Siwezi kusema sana juu ya mechi dhidi ya Yanga
itakavyokuwa kwa sababu mimi siyo mzungumzaji mno ila nitakachokifanya ni
kutenda uwanjani kama ninavyofanya kwenye mechi nyingine za timu yangu.
“Mechi itakavyokuwa vyovyote kwangu sawa kwa
sababu nipo tayari na nimejiandaa kucheza na sina wasiwasi ila kwa wale ambao
watataka kuona nitafanya nini basi waje kuona uwanjani na siyo kuanza kuongea
sana kabla mechi yenyewe haijachezwa,” alisema Mavugo anayetumia jezi namba 11
katika kikosi hicho.
Post a Comment