Haikuwa ubashiri, badala yake ilikuwa
ni mipango thabiti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha
kwamba inavuna ushindi na kuwa mabingwa wa Kombe la Chalenji la CECAFA kwa
wanawake baada ya kuilaza Kenya mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika
Uwanja wa Nambole jijini Jinja nchini Uganda.
Mabao ya timu ya taifa Tanzania ya
wanawake maarufu kama Kilimanjaro Queens katika mchezo wa leo Septemba 20, 2016
yamefungwa na Mwanahamisi Omari katika kipindi cha kwanza kabla ya Kenya
kujitutumua na kupata bao la kufutia machozi kipindi cha pili katika mchezo
uliokuwa na ushindani wa aina yake.
Matokeo hayo yatakuwa kupozwa kwa
ndugu zao wa Zanzibar Queens ambao walitolewa mapema katika mashindano hayo
yaliyoanza Septemba 11, 2016 kabla ya kufikia tamati leo katika fainali hizo
zilizovutia mashabiki wa mpira wa miguu nchini Uganda ambako kila upande
ulikuwa na watu wanaowasapoti.
Timu hiyo inatarajiwa kuondoka nchini
Uganda kesho Jumatano na kwenda moja kwa moja Kagera ambako ilipiga kambi kabla
ya kwenda Jinja. Itarudi hapo kusema ahsante kwa wenyeji, lakini pia kuwapa
pole ya janga la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na mikoa
jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi ni
Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.
Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo
itasafiri kutoka Kagera kwa usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo
zitatangazwa na TFF hapo kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na
kuishangilia timu hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiwa na Hilda
Masanche wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake.
Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro
Queens ulianzia hatua ya makundi kwa kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka
sare tasa na Ethiopia ambayo pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa
Rwanda. Tanzania na Ethiopia zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania
ikawa ya kwanza katika kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao
4-0 katika mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa
mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.
Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania,
Burundi, Zanzibar, Kenya, Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda.
Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa
mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka
la wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati
Post a Comment