YANGA wameuchungulia msimamo wa Ligi
Kuu Tanzania Bara, wakagundua kuwa wapo nafasi ya tatu, na sasa wanaondoka
kesho kuelekea Shinyanga kuwavaa Mwadui FC, huku wakiwa na kikosi cha
maangamizi.
Kocha Mkuu wa mabingwa hao watetezi,
Hans Pluijm, ameahidi kuendeleza ubabe na kukisambaratisha kikosi cha kocha
mwenye maneno mengi, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, katika uwanja wao wa nyumbani
uliopo Mwadui, Shinyanga.
Katika msimamo wa Ligi hiyo, Yanga
wanashika nafasi ya tatu, wakiwa na pointi saba katika michezo yao mitatu
waliyokwisha kucheza mpaka sasa, huku Azam na Simba zikikabana koo kileleni
kila moja ikiwa na pointi 10, wao wakiwa wamecheza michezo minne.
Yanga wanaondoka kesho wakiwa na kauli
moja tu ambayo kwa sasa imesambaa mitaani ya kusepa na kijiji, wakimaanisha
kuwa itabidi mabeki wa Mwadui wajizatiti, kwani safu ya ushambuliaji
inayoongozwa na Donald Ngoma na Amis Tambwe itakuwa na kasi ya ajabu.
Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa
na hasira kali kutokana na kumbukumbu ya kutoka sare ya kufungana mabao 2-2
katika mchezo wa msimu uliopita, uliochezwa katika Uwanja wa Kambarage, mkoani
humo.
Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka
Deusdedit, amesema kuwa wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wale waliokuwa
wakizitumikia timu zao za Taifa, akiwamo Haruna Niyonzima na Vicent Bossou,
wameshawasili na kuungana na wenzao tayari kwa kutafuta pointi tatu muhimu.
“Niseme tu kwa upande wetu kama
uongozi kila kitu kipo sawa, japo siwezi kusema kwamba tunaondoka lini,
wachezaji wote wapo katika hali nzuri na benchi letu la ufundi linafanya kazi
yao ipasavyo,” alisema.
Akizungumzia mchezo huo, alisema licha
ya changamoto zinazowakabili, ikiwamo uchovu wa wachezaji baada ya kutumika kwa
muda mrefu, hasa kwenye michuano ya kimataifa iliyokuwa ikiwakabili,
watahakikisha wanaondoka na pointi tatu.
“Kuna changamoto nyingi, kwani kama
unavyojua wachezaji wetu walitumika sana, ila yote kwa yote Yanga ni timu kubwa
na kila tutakapofika tutaondoka na pointi tatu,” alisema.
Katika mchezo huo, Yanga itawategemea
sana washambuliaji wake Donald Ngoma, Amis Tambwe ambaye ni mfungaji bora wa
msimu uliopita pamoja na Obrey Chirwa, ambao wanatarajiwa kuwakimbiza vilivyo
mabeki wa Mwadui FC.
Kwa upande wa safu ya ulinzi, Vicent
Bossou anatarajiwa kuwaongoza wenzake kama alivyoiongoza timu yake ya Taifa ya
Togo kutinga michuano ya AFCON, huku Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima
wakitawala eneo la katikati.
Post a Comment