KIUNGO mkabaji
wa Yanga, Mzimbabwe, Thabani Kamusoko, juzi Jumamosi aliugua ghafla ugonjwa wa
kiungulia na kushindwa kumaliza mechi dhidi ya Mwadui FC.
Yanga ilivaana
na Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara
iliyomalizika kwa timu hiyo kushinda mabao 2-0 yakifungwa na Amissi Tambwe na
Donald Ngoma.
Daktari mkuu
wa timu hiyo, Edward Bavu, alisema kiungo huyo alishindwa kumalizia mechi na
Mwadui baada ya kupata kiungulia ghafla katikati ya mchezo huo.
Bavu alisema
wamegundua tatizo baada ya kumfanyia vipimo, hivyo tayari amempatia matibabu na
hivi sasa anaendelea vizuri na mechi ijayo dhidi ya Stand United atakuwepo
uwanjani.
Aliongeza
kuwa, beki wao wa kati raia wa Togo, Vincent Bossou, amepona malaria na
anaendelea vizuri baada ya kumpatia matibabu, naye mechi ijayo atakuwepo kama
kocha akihitaji kumtumia.
"Kamusoko
anaendelea vizuri, mechi ya jana (juzi) alishindwa kuendelea na mechi katika
kipindi cha kwanza baada ya kuugua ghafla kiungulia.
"Alikuwa
ana uwezo wa kuendelea mechi na Mwadui, lakini nikashauri kumpumzisha kwa hofu
ya kiafya baadaye lisije likatokea tatizo kubwa.
"Kwa
sababu tatizo hilo alilolipata wakati mwingine linatokana na tatizo la moyo na
chakula ambacho mchezaji amekula, hivyo nikashauri tumtoe kwa ajili ya vipimo
zaidi," alisema Bavu.
Post a Comment