KUTOKANA na fununu zinazoibuka kila kukicha juu ya
kuhitajika kwa beki wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ au Zimbwe Jr kwenda
timu nyingine, uongozi wa Wekundu hao umeamua kuweka wazi dau la mchezaji huyo
kwa timu inayotaka kumnunua.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans
Poppe ametamka kuwa kulingana na kiwango na mchango alionao mchezaji huyo,
thamani yake kwa timu yoyote itakayomtaka kwa sasa ni dola 600,000 (zaidi ya
shilingi bilioni 1.3), ambapo kikitolewa kiwango hicho wao wapo tayari kumpa
ruhusa kuondoka.
Mchezaji huyo amekuwa akitajwa
kuwaniwa na Yanga hivi karibuni, hivyo hiyo ni kama kutangaziwa dau mapema na Wekundu
hao kwamba kama wapinzani wao hao watahitaji huduma ya mchezaji huyo lazima watoe
kitita hicho na kuweka rekodi ya usajili Bongo kwani haijawahi kutokea.
“Kijana anafanya kazi nzuri kwa sasa, kila mmoja anaiona, tumesikia
kuwa kuna klabu zinamtaka na si vizuri kumfuata yeye mwenyewe kwa kuwa bado yupo
ndani ya mkataba.
“Sasa kutokana na kiwango na mchango alionao ndani ya timu, kwa
klabu yoyote itakayomhitaji, thamani yake ni dola laki sita. Soka limefikia
huko kwa sasa.“Miaka ya nyuma ilikuwa dola 80,000, dola laki moja au mbili lakini
soka limebadilika sasa na ukiangalia mchezaji kama huyu anayefanya kazi yake
sawasawa hilo ndiyo dau lake kwa timu yoyote itakayomtaka kwa ajili ya huduma
ya uwanjani,” alisema Poppe.
Tshabalala ambaye alijiunga na timu hiyo msimu wa 2014/15 akitokea
Kagera Sugar, amebakiza mwaka mmoja klabuni hapo huku kiwango chake kikizidi
kukua kila kukicha akiwa na wastani wa kutoa asisti tatu katika mechi nne walizocheza
mpaka sasa msimu huu.
Katika kutambua mchango wa beki huyo wa kushoto anayetajwa kusajiliwa
Simba kwa Sh milioni 12 akitokea Kagera, mwanzoni mwa wiki hii, Hans Poppe alimzawadia
gari aina ya Toyota Raum ikiwa kama zawadi kwa kazi yake nzuri muda wote akiwa katika
kikosi hicho.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, beki huyo alisema: “Siwezi kuzungumza
suala lolote kuhusu usajili au mkataba wangu, hilo ni suala ambalo lipo kwa
meneja wangu, unaweza kuwasiliana naye.”
Alipotafutwa mmoja wa watu wanaomsimamia Tshabalala, Heri
Mzozo hakupatikana kwa kuwa simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa kwa muda
mrefu.
Post a Comment