BEKI wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’, amevunja rekodi ya mabeki wakongwe wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani ya kucheza mechi tatu mfululizo za ligi bila ya kuruhusu bao.
Dante aliyejiunga na Yanga akitokea Mtibwa Sugar kwa mkataba wa miaka miwili, tayari ameonyesha uwezo mkubwa katika nafasi ya beki wa kati kutokana na kuhimili mikikimikiki na kutoruhusu bao lolote katika michezo waliyocheza mpaka sasa.
Beki huyo mechi yake ya kwanza dhidi ya African Lyon waliyoibuka na ushindi wa mabao 3-0 alicheza sambamba na Vincent Bossou raia wa Togo kabla ya kucheza mechi mbili dhidi ya Ndanda na Majimaji sambamba na Cannavaro. Matokeo ya mechi hizo yalikuwa ni suluhu na ushindi wa mabao 3-0.

Msimu uliopita katika mechi tatu za kwanza ambazo Yanga ilicheza huku safu ya ulinzi ikiongozwa na mabeki wa kati, Yondani na Cannavaro, walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union, wakaifunga Tanzania Prisons mabao 3-0, kabla ya kuruhusu bao moja katika mchezo wa tatu na JKT Ruvu uliomalizika kwa kushinda mabao 4-1.
Kutokana na rekodi hiyo ya Dante, Yanga imefanikiwa kufikisha pointi saba na mabao sita nyuma ya vinara wa ligi hiyo Azam wanaoongoza kwa pointi kumi wakifunga mabao saba.

Post a Comment

 
Top