KOCHA wa zamani wa Vital’O ya nchini
Burundi, Etienne Ndayigije, ambaye amewahi kuwafundisha Laudit Mavugo wa Simba
na Amis Tambwe wa Yanga, ameweka wazi kuwa straika huyo mpya wa Wekundu wa
Msimbazi ataibuka mfungaji bora.
Kocha huyo, ambaye kwa sasa
anaifundisha Mbao FC ya mkoani Mwanza, alisema wachezaji hao wote wawili wana
uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu na huenda Mavugo akafanikiwa katika mbio hizo
za ufungaji bora, kwani ana uchu wa mabao.
Alisema kama Tambwe aliweza kuibuka
mfungaji bora msimu wake wa kwanza alipokuwa akiichezea Simba, haitashindikana
kwa Mavugo, ambaye amekuja nchini Tanzania akiwa mfungaji bora Ligi ya nchini
Burundi.
“Tambwe na Mavugo wote wamepita katika
mikono yangu, nawajua vizuri sana, ndiyo maana nasema ushindani wa kutafuta
mfungaji bora utakuwa mgumu sana, hasa kwa hawa vijana wangu wawili.
“Msimu wa kwanza kwa Tambwe aliweza
kuchukua ufungaji bora na sasa nadhani itakuwa zamu ya Mavugo, ndivyo
ninavyowaza mimi, japo hata Tambwe anaweza akafanikiwa kutetea heshima yake
hiyo,” alisema.
Alisema licha ya kwamba kwa sasa
wanakimbizana kila mmoja akiwa na mabao matatu, anaona Tambwe anaweza akachoka
kadri ligi itakavyokuwa inaendelea kutokana na kutumika sana, ikiwamo michuano
ya Kimataifa iliyokuwa ikiwakabili Yanga.
“Nadhani Tambwe ametumika sana,
ikiwamo michuano ya kimataifa, tofauti na Mavugo, sasa hiyo inaweza kumchosha
kadri ligi itakavyokuwa ikiendelea,” alisema.
Msimu uliopita Tambwe aliibuka
mfungaji bora nchini Burundi akiwa na Vital’O, akifanikiwa kufunga mabao 32,
huku Tambwe akifunga mabao 21 na kuibuka mfungaji bora Ligi Kuu Tanzania Bara
na sasa kila mmoja anataka kumuonyesha mwenzake umwamba.
Post a Comment