Rais wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameshitushwa na taarifa za
tukio la tetemeko kubwa ardhi lenye mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7
lililotokea jana Septemba 10, 2016 katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa
kadhalika nchi za Burundi na Uganda.
Mikoa ya
Kanda ya Ziwa iliyopata athari kwa mujibu wa taarifa ni Mwanza, Mara na Kagera
nchini na kuripotiwa kuua zaidi ya watu 10 na wengine zaidi ya 120 kujeruhiwa
sambamba na kubomoa majengo mbalimbali.
Rais Malinzi
mara moja anaungana na Serikali katika kusubiri tathmini na kisha kuangalia
namna TFF itakavyoweza kusaidia kama sehemu ya wadau katika jamii. TFF inaamini
kuwa baadhi ya waliopata maafa ni familia ya mpira wa miguu si ndani tu ya
nchi, bali pia nje ya mipaka ya Tanzania.
Hivyo, Rais
Malinzi ametutuma salamu za rambirambi kwa familia zote zilizopoteza ndugu,
jamaa na marafiki na anawaombea marehemu wapumzishwe mahali pema peponi. Amina.
Na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira na uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu.
Katika
salamu hizo, pia Rais Malinzi amemtumia Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu
Burundi (BFF), Marlon Kuylen kwa sababu sehemu ya Bujumbura imeguswa na
tetemeko hilo kadhalika ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Moses Magogo baada ya ripoti kuonesha kuwa
tetemeko hilo limeukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda. Wataalamu wa
elimu ya miamba – Jiolojia wanasema kwamba lilikuwa ni kubwa kwa mujibu wa
vipimo.
Post a Comment