STAND United imesema Yanga itaumbuka vibaya, baada kukata rufani kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa madai timu hiyo ilimchezesha Frank Khamis Igobela kimakosa katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mechi hiyo iliyopigwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga, Yanga ilifungwa bao 1-0 na kwa sasa wamepiga hodi kwa shirikisho hilo na madai kuwa Stand United ilimtumia Igobela pasipo kufuata taratibu za usajili.
Yanga imedai kuwa, Stand United ilimtumia Igobela huku akiwa bado ni mchezaji halali wa Polisi ya visiwani Zanzibar na hakuwa na leseni.
Baada ya Yanga kuwasilisha barua ya madai yao kwa TFF, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Stand United, Mbassa Mong’ateko, ameshangazwa na taarifa hizo ambazo amesema hazina ukweli wowote.
Mong’ateko alisema Igobela ni mchezaji wao halali baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu tangu msimu uliopita wa 2015/16.
Mwenyekiti huyo alisema Igobela alikuwa katika kikosi kilichopita na alifunga mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara.
“Tunashangazwa na hizi taarifa zisizo na ukweli na kama kweli Yanga wamepeleka barua ya kupinga kumtumia Igobela watakuwa wanapoteza muda, kwani ni mchezaji wetu halali kwa msimu wa pili sasa, lakini akiwa amebakiwa na mkataba wa mwaka mmoja kati ya mitatu tuliyompa msimu wa 2015/16.
“Iwapo msimu uliopita aliweza kuichezea timu yetu mechi za ligi, ikiwemo zile mbili za Yanga, leo amekuwaje mchezaji wa Polisi Zanzibar, lakini yote hayo tunasubiri TFF watuite ili tupeleka utetezi wetu juu ya Igobela,” alisema.
Spotiripota ilimtafuta Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, ili kujua kama wamepata barua ya Yanga, alisema hajaiona mezani kwao.
Post a Comment