KIKOSI cha Yanga kimeshindwa kuwapa raha mashabiki wake waliojitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga baada ya kuambulia kichapo cha bao 1-0.
Stand inayonolewa na Kocha Mfaransa, Patric Liewig, ilionekana kutafuta bao mapema lakini ilikosa nafasi kadhaa za wazi na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikishambulia kwa zamanu, alikuwa ni Pastory Athanas katika dakika ya 58 ambapo alifanikiwa kuiandikia Stand bao la kuongoza na pekee akiwazidi ujanja walinzi wa Yanga, Hajji Mwinyi ambaye ndiye aliyekuwa na uwezo wa kuufikia mpira.
Mwinyi ambaye alionekana kujiamini zaidi alichelewa kuuwahi mpira ambao ulikuwa mbele yake kidogo kabla ya Pastory kutokea nyuma na kuuwahi na kupiga shuti la chini ndani ya 18 lililomshinda kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na kisha kuingia uwanjani.
Baada ya mchezo huo kumalizika mchezaji Jacob Massawe wa Stand United alisema: “Yanga walikuwa wepesi sana, tuliwaangalia kwenye mechi yao waliyocheza na Mwadui (Yanga ilishinda 2-0) tukaona wana upungufu mkubwa sisi tukaenda kuufanyia kazi, leo ilikuwa tupige bao nyingi lakini sema hatukutumia nafasi tulizopata.”

Post a Comment

 
Top