HIVI karibuni Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon,
Joseph Omog, alikuwa na kazi kubwa ya kuwafua mabeki wake hususan wale wa kati
ili waweze kuwa fiti tayari kwa kukabiliana na washambuliaji wa Yanga, Mrundi,
Amissi Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma.
Washambuliaji hao walikuwa wakimkosesha usingizi
kocha huyo kila alipokuwa akiifikiria kazi yao wanapokuwa uwanjani wakifosi
kupata ushindi.
Hali hiyo lilimfanya achukue jukumu la kuwafua
vilivyo mabeki wake ili wawe tayari kukabiliana na washambuliaji hao Jumamosi
hii, jambo ambalo amedai kuwa limefanikiwa kwa kiwango cha juu.
Omog alisema kuwa hana tena hofu yoyote kuhusiana
na washambuliaji hao baada ya kuridhishwa na uwezo mkubwa wa mabeki wake ambao
wamekuwa wakiuonyesha mazoezini tangu alipoanza kuwafua kwa ajili ya mchezo huo
lakini pia mechi nyingine za ligi kuu.
“Sina hofu yoyote tena juu ya washambuliaji hao
kwani hivi sasa nawaamini vilivyo mabeki wangu kutokana na uwezo wao mkubwa
ambao wamekuwa wakiuonyesha mazoezini.
“Wameiva vilivyo na wapo vizuri na wapo tayari
kukabiliana na washambuliaji hao kwa mpira wa aina yoyote ile, iwe kwa mipira
ya juu au chini. Hakuna njia ya kupita kirahisi,” alisema Omog na kuongeza kuwa
katika harakati zake hizo za kuwafua mabeki wake hao, amevutiwa zaidi na
kiwango cha Mganda, Juuko Murshid, hivyo anaweza akamtumia katika mchezo huo
unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi na mashabiki wa soka hapa nchini.
Endapo Juuko atafanikiwa kuwa katika kikosi cha
kwanza cha Simba siku hiyo, basi itakuwa ni mara yake ya pili tangu ligi hiyo
ilipoanza kutimua vumbi msimu huu ambapo mara yake ya kwanza kuanza kuwa katika
kikosi cha kwanza cha timu hiyo ilikuwa juzi Jumamosi dhidi ya Majimaji FC.
Mabeki ambao mara kwa mara wamekuwa wakiongoza
Simba msimu huu ni Mzimbabwe mwenye asili ya Tanzania, Method Mwanjale na
Novaty Lufunga.
Post a Comment