YANGA imekuja na mikakati mizito ya kuhakikisha wanashinda michezo yao yote baada ya kuamua kuikabidhi timu hiyo kwa vigogo ambao watakuwa wanaambatana nayo kila inapokwenda.
Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wanaondoa mianya yote ya hujuma zikiwemo zile za ndani na nje ya uwanja katika michezo yao mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakianzia na mechi yao ya ugenini dhidi ya Mwadui FC.
Hii imekuja baada ya kiongozi wa juu wa klabu hiyo kutoa kazi maalumu kwa kamati yake ya mashindano ambayo ameitaka kuhakikisha kila timu hiyo inapokuwa na mechi kunakuwa na wajumbe wawili wa kuhakikisha ushindi unarudi Jangwani.
Kamati hiyo mpya imeundwa karibuni baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wake, Issac Chanji na sasa iko chini ya Uenyekiti wa Mhandisi Paul Malume.
BINGWA lina taarifa kuwa tayari vigogo wawili wa kamati hiyo wameshateuliwa kusafiri na timu kwa ajili ya kuhakikisha timu hiyo inarudi Shinyanga na pointi zote sita.

Chanzo cha habari cha BINGWA kililiambia gazeti hili kuwa vigogo wawili walioteuliwa kuambatana na timu hiyo kwa ajili ya safari ya Shinyanga ni Yusuphedi Mhandeni na Jackson Mahagi ambao watakaa na timu hiyo mkoani humo kwa wiki nzima ambapo itacheza na Mwadui na Stand United.
Mnyetishaji wetu aliendelea kufunguka kuwa baada ya wawili hao kutimiza majukumu yao kwenye safari ya Shinyanga, watapokewa na wengine katika michezo inayofuata yote hiyo ikiwa ni katika harakati za kuziba mianya yote ya hujuma.
Wajumbe wengine watakaopokezana kwenye safari hizo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Mhandisi Paul Malume, Abdallah Bin Kleb, Mustafa Ulungo, Mhandisi Mahende Mugaya, Jackson Mahagi, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
Wengine ni Athumani Kihamia wa Arusha, Felix Felician Minja wa Mwanza, Leonard Chinganga Bugomola wa Geita, Omar Chuma, Hussein Ndama, Hamad Ali Islam wa Morogoro, Yusuphedi Mhandeni, John Mogha, Beda Tindwa, Moses Katabaro na Roger Lemlembe.

Mbali na uamuzi huo wa kuwataka vigogo kuambatana na timu kila inapokwenda, kamati hiyo imeangalia kasi ya Azam na Simba na kushtukia kuwa kuna uwezekano ligi ikaja kuamuliwa na mabao ya kufunga na kufungwa.
Hivyo basi wamewataka wachezaji na benchi la ufundi kuhakikisha timu inakuwa inapata matokeo ya mabao mengi ili ikifika wakati ligi ikaamuriwa na mabao ya kufunga na kufungwa wawe kwenye wakati mzuri.
Inadaiwa kuwa viongozi wa juu wa klabu hiyo wamelionya benchi la ufundi na kulitaka kuhakikisha Yanga inaepukana na sare za ‘kibwege-bwege’ kwa sababu wanaamini kikosi chao ni bora zaidi kwa Tanzania kwa sasa na hakuna timu ya kukizuia.
Kikosi cha Yanga leo kinatarajia kwenda mkoani Shinyanga kwa ndege kwa ajili ya pambano lao dhidi ya Mwadui ambalo litapigwa mwishoni mwa wiki hii.

Post a Comment

 
Top