WAKATI leo Jumamosi jioni Yanga
ikitarajiwa kucheza na Majimaji katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa,
mabosi wa timu hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao, Yusuf Manji juzi Alhamisi
usiku walikutana ghafla na wachezaji wa kikosi hicho kupanga mikakati ya
ushindi.
Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya
wachezaji hao kuwasili jijini Dar es Salaam wakitokea Mtwara walipokuwa wamecheza
na Ndanda FC.
Jumatano wiki hii, Yanga ilitoka
suluhu na Ndanda ugenini mkoani Mtwara kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona na
kuonekana kama kasi yao imepunguzwa.
Kabla ya kutoka sare hiyo, Yanga
ilikuwa imeifunga African Lyon mabao 3-0 katika mechi yake ya kwanza ya Ligi
Kuu Bara.
Katika kikao hicho kilichofanyika
kwenye hoteli moja iliyopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi, Manji akiwa na
viongozi wote wa Kamati ya Mashindano walikutana na wachezaji na benchi zima la
ufundi la Yanga.
Manji na mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhandisi
Paul Malume, walikutana na wachezaji hao ili kuweka mikakati ya kutetea ubingwa
wao wa ligi kuu baada ya kuona wametoka suluhu na Ndanda.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari
kilichokuwepo hotelini hapo, kikao hicho kilianza saa 2:30 usiku na kilitumia
muda wa saa moja ambapo wachezaji walipewa ahadi mbalimbali ili waweze kupata
ushindi.
“Tulikuwa tunaweka mikakati maana ile
sare ya Ndanda kidogo imetufanya tushtuke natumekubaliana baadhi ya mambo na
wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
“Utekelezaji wa mambo hayo unaanza
katika mechi yetu na Majimaji kesho (leo) Jumamosi, tunataka kushinda mechi hii
na nyinginezo ili tuweze kutetea ubingwa.
“Wachezaji wamepewa
motisha mbalimbali zitakazowafanya wafanye vizuri uwanjani kwani licha ya
kutambua kuwa ni jukumu lao lakini lazima tukubali ligi ni ngumu,” kilisema
chanzo hicho.
Post a Comment