Hivi karibuni
kiungo wa pembeni wa Yanga, Deus Kaseke amekuwa akitumika kama kiungo wa kati
wa timu hiyo akichukua majukumu ya Haruna Niyonzima ambapo Kocha wa Yanga, Hans
van Der Pluijm ameeleza kuhusiana na majukumu hayo huku akitoa sababu za
kumzoesha Kaseke kucheza nafasi hiyo.
Kaseke
ameitumikia nafasi hiyo kwa mechi mbili mfululizo sasa baada ya kukosekana kwa
Niyonzima aliyekuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Rwanda. Mechi ya kwanza
ilikuwa dhidi ya Ndanda iliyoisha kwa suluhu, ya pili ni ya Jumamosi iliyopita
walipoifunga Majimaji 3-0.
Pluijm amekiri
kufurahishwa na uchezaji wa Kaseke katika nafasi hiyo ingawa alikuwa na uwanja
mpana wa kuchagua viungo wa kati wengine ambao wangeweza kucheza na Mzimbabwe,
Thabani Kamusoko eneo la kati.
“Kaseke safi
sana, anacheza vizuri akiwa kati, anapambana, anajituma na anajua afanyeje
akiwa katika majukumu ya kiungo wa kati. Ndiyo wapo wachezaji wenye uhalisia wa
nafasi hiyo ambao ningeweza kuwapanga lakini unaangalia nani anaweza kuziba
vizuri pengo kulingana na mfumo,” alisema Pluijm raia wa Uholanzi na kuongeza:
“Kwa baadaye
siwezi kujua kama Kaseke anaweza kuhamia katika nafasi hiyo moja kwa moja
lakini ni jambo muhimu kumzoesha mchezaji kama huyu ambaye anaweza kusimama
nafasi mbalimbali na akacheza kwa asilimia kubwa au kuliziba kabisa tatizo.”
Katika majukumu
yake hayo mapya, Kaseke alifanikiwa kufunga bao moja juzi katika mechi ya
Majimaji likiwa ni bao lake la pili msimu huu baada ya awali kufunga dhidi ya
African Lyon.
Post a Comment