KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm, amemtaja  Juma Mahadhi kama ‘Super Sub’ wake, baada ya staa huyo wa zamani wa Coastal Union kuingia na kubadili mchezo dhidi ya Majimaji, akichukua nafasi ya Mzambia, Obrey Chirwa.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru (Shamba la Bibi), jijini na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, Mahadhi alionyesha kiwango cha juu baada ya kuingia uwanjani katika kipindi cha pili.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Pluijm alisema kuwa mastraika wake walipoteza nafasi nyingi kwenye kipindi cha kwanza, lakini baada ya kuingia Mahadhi alifanikiwa kubadilisha mchezo na kuisaidia timu kupata mabao mawili ya haraka.

Alisema Mahadhi aliongeza kasi ya mchezo na kupeleka mashambulizi zaidi mbele, kitu ambacho alikuwa anahitaji kifanyike.
Alisema licha ya usumbufu walioupata kutokana na kutozoea kucheza mechi kwenye uwanja wa nyasi bandia na kupelekea mipira kwenda sana, lakini ushindi huo umewaongezea ari wachezaji wake ili kuendelea kufanya vizuri kwa michezo inayowakabili mbele yao.
Baada ya ushindi huo Yanga imefikisha pointi saba baada ya mechi tatu, ikiwa nyuma ya Azam na Simba zilizo juu ya msimamo huo zikiwa na pointi 10 kila moja baada ya mechi nne.
Yanga wanatarajiwa kuwa wageni wa Mwadui FC katika mechi yao inayofuata, itakayopigwa Septemba 17, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Post a Comment

 
Top