BAO la dakika za majeruhi lililofungwa na straika
wa Yanga, Donald Ngoma, juzi Jumamosi, limemkuna kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelo
‘Julio’ na kushindwa kuficha hisia zake baada ya kutamka: “Ngoma amefunga bao
kali sana.”
Ngoma alifunga bao hilo katika dakika nne za
nyongeza baada ya zile tisini kukamilika kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi
ya Mwadui uliopigwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na kumalizika kwa Yanga
kushinda 2-0. Bao lingine lilifungwa na Amissi Tambwe dakika ya tano.
Kabla ya mchezo huo, Julio alikuwa akiwabeza
washambuliaji wa Yanga, hasa Ngoma na Tambwe ambapo alitamba vijana wake
watawadhibiti na kushindwa kufurukuta, lakini haikuwa hivyo.
Akilizungumzia bao hilo ambalo liliihakikishia
Yanga ushindi na kukwea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu kwa
kufikisha pointi kumi, Julio alisema:
“Mazingira ya bao lenyewe yalikuwa hivi; Msuva
aliingia na mpira kwenye eneo letu la hatari, akaona hawezi kupiga krosi,
akamuachia Niyonzima ambaye alipiga krosi iliyounganishwa na Ngoma kwa kichwa
safi, niseme tu Ngoma amefunga bao zuri mimi mwenyewe nimelikubali.
“Lakini bao la kwanza ni uzembe tu wa mabeki
wangu kushindwa kuokoa hatari na kumpa mwanya Tambwe kufunga bao la uongozi
kabla ya hilo la pili.”
Ikumbukwe kuwa, msimu uliopita timu hizo
zilipokutana kwenye uwanja huo, zilitoka sare ya mabao 2-2 ambapo Ngoma
aliifungia Yanga mabao yote huku ya Mwadui yakifungwa na Paul Nonga na Bakari Kigodeko.
Post a Comment