BEKI wa Medeama, Daniel Amoah, aliyesajiliwa na Azam msimu huu juzi aliwapagawisha viongozi wa klabu hiyo ya Chamazi kutokana na uwezo wake wa kucheza namba zaidi ya moja pale alipoanza kucheza kwa mara ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.
Beki huyo ambaye katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Yanga alisababisha Tambwe kutolewa uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mahadhi wakati timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1. Yanga ilifungwa mabao 3-1 katika mchezo wa marudiano nchini Ghana.
Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine uliomalizika kwa Azam kuondoka na ushindi wa bao 1-0 walilolipata kupitia kiungo wao, Michael Bolou.
Kwenye mchezo huo, Amoah alionyesha kiwango cha hali ya juu ambapo alianza kupangwa kama beki ya kulia kabla ya kucheza ‘sentahafu’ kipindi cha pili.
Kufuatia kiwango hicho, kocha mkuu wa timu hiyo, Zeben Hernandez, alisema amefarijika na viwango vya nyota huyo kutoka Ghana.
Zeben alitoa sifa pia kwa mshambuliaji wake kutoka Ivory Coast, Gonazo Thomas ambaye pia alicheza kwa mara ya kwanza.
“Nimefarijika na viwango walivyovionyesha kwenye mechi hii ya kwanza toka wasajiliwe, nina imani watakuwa msaada kwenye kikosi hiki,” alisema.
 Katika hatua nyingine, kocha huyo alisema anaendelea na maandalizi ya mechi inayofuata dhidi ya Mbeya City keshokutwa.

Post a Comment

 
Top