MASAU Bwire ameshaanza tambo zake kuelekea mchezo wao wa keshokutwa Jumatano dhidi ya Simba.
Msemaji huyo wa Ruvu Shooting, ameipiga dongo Simba akisema ijiandae na kipigo katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar huku akienda mbali zaidi kwa kusema siku hiyo straika Laudit Mavugo atatulizwa na mashabiki kumuita kinyozi.
Bwire alifunguka kuwa hawatishwi na mabadiliko yaliyofanywa na Simba, kwa kuwa bado hawajashindana na timu zenye uwezo mkubwa huku akimchambua Mavugo kuwa ni wa kawaida.


“Unajua tatizo watu wanakwenda na historia ya majina kwamba mtu alikuwa maarufu kipindi hicho sasa wanataka aendelee kuwa hivyo, hata kama uwezo wa kufanya hivyo haupo, ila sisi hatubahatishi na kutokuwepo kwa George Michael siyo kwamba ndiyo tumetetereka kwa sababu watu hawawajui wachezaji wetu ila wakiwaona wenyewe watasaluti.
“Tunajua kwamba sasa hivi ukipita sehemu unasikia Mavugo lakini tunataka kuonyesha kuwa wapo zaidi ya huyo Mavugo na siku hiyo pengine mashabiki wa Simba wakosee kuita jina la Mavugo na kumuita kinyozi kutokana na shughuli atakayokutana nayo, haitakuwa ndogo kutokana na ubora wetu,” alisema Bwire.

Post a Comment

 
Top