SIMBA wamechungulia beki yao ya kulia wakagundua kuwa kuna mapungufu makubwa na sasa wameamua kumrejesha beki wao wa zamani, Shomari Kapombe, aliyepo Azam FC.
Licha ya kwamba Simba inao mabeki watatu katika nafasi hiyo, lakini wanaona kuwa hawana ile kasi wanayoitaka kama ya Shomari Kapombe na sasa wanataka kumrejesha mkali wao huyo.
Katika misimu iliyopita Simba ilifanikiwa kuwa na mabeki wakali wa kulia, ambao walikuwa na uwezo wa kupandisha mashambulizi, kupiga krosi za maana na kurudi haraka kuzuia, lakini sasa wanaona kuna upungufu huo.
Mabeki hao wa zamani waliokuwa na kasi hiyo ya ajabu ni pamoja na Nassor Masoud ‘Chollo’, Salum Kanon, Shomari Kapombe na msimu uliopita alikuwepo Hassan Ramadhan ‘Kessy’ ,ambaye kwa sasa yupo Yanga.
Kwa sasa mabeki ambao wapo ni Mcongo Javier Bukungu, Hamad Juma pamoja na Malika Ndeule, ambao licha ya uwezo walionao, wanatajwa kupungukiwa na kasi ya kupandisha mashambulizi na kupiga krosi za uhakika.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa umesukwa mpango kabambe kuhakikisha wanamrejesha Shomari Kapombe, dirisha dogo la usajili.
 Kigogo mmoja wa Simba ameliambia DIMBA Jumatano, kuwa wamejipanga kumrejesha beki wao huyo wa zamani, ikizingatiwa kuwa kwa sasa suala la fedha si tatizo kwao.
“Ni kweli hizo taarifa ni za kweli kabisa, tunataka kumrejesha Kapombe, kwani tumeona kuna mapungufu katika nafasi ya beki wa kulia, hawa waliopo ni wazuri, lakini kuna vitu vichache wanamisi.
“Unajua sasa hivi hatuna wasiwasi wa namna ya kupata fedha, kwani kila mtu unayemgusa yupo radhi kuisaidia timu, sasa hilo jambo linaweza likawa rahisi, tunatarajia kumchukua dirisha dogo na kama ikishindikana sana tutamsubiri msimu ukimalizika,” alisema.

Post a Comment

 
Top