Ajib, Mavugo waja kivingine
WALE mabeki wa timu pinzani ambao wamekaririshwa kumbana straika wa Simba, Laudit Mavugo asifunge, imekula kwao kwani Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi hao, Joseph Omog, amekuja na mbinu mbadala itakayowawezesha wawili hao kuwaliza wapinzani wao.
Omog amegundua hilo na kulifanyia kazi ambapo anaamini kwamba mabeki wa timu pinzani wakimkaba sana Mavugo, basi kuna wachezaji wake wengine watafunga.
Katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara aliyocheza ikiwamo dhidi ya Ndanda FC, JKT Ruvu na Ruvu Shooting, Mavugo amekuwa na kazi kubwa kutokana na mabeki wa timu pinzani kuingia uwanjani wakiwa na maelekezo maalumu ya kumkaba mshambuliaji huyo.
Omog aliwatumia Mavugo na Ibrahim Ajib katika kikosi cha kwanza katika safu yake ya ushambuliaji ambapo wakati mabeki wa timu pinzani wakiwa makini kumzuia Mavugo kutoleta madhara, Ajib alipata fursa ya kufanya kweli.
Hali kadhalika, pale mabeki wanapohamia kwa Ajib, Mavugo anapata mwanya wa kuwaliza kama ilivyojitokeza katikati ya wiki katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ulioishia kwa Simba kushinda mabao 2-1.
Baada ya Omog kubaini mtindo ambao anaweza kuutumia kwa Ajib na Mavugo ili kuziadhibu timu pinzani, kocha huyo amebuni mbinu mbadala za kuwawezesha kuvuna mabao katika mechi zao na hatimaye kuzoa pointi zote tatu.
Omog alisema alibaini hilo baada ya kuona mechi dhidi ya Ruvu Shooting ambapo Mavugo alikuwa katika wakati mgumu kutokana na kukaba na kuangaliwa zaidi.
Alisema licha ya kupoteza umakini katika ufungaji lakini mabeki wa Ruvu Shooting walimwondoa mchezoni mchezaji wake huyo na kufikia hatua ya kumuumiza.
Alisema ameliona jambo hilo la mabeki kuingia uwanjani kwa maelekezo ya kuwakaba baadhi ya wachezaji akiwemo Mavugo ambaye wanaamini ni tegemeo kubwa katika nafasi ya washambuliaji.
“Ninaendelea kuwanoa washambuliaji wangu wote pamoja na viungo kwa kuwapa saa kwa ajili ya kutengeneza umakini pamoja na mbinu za mabeki ambao wanakuja kwa lengo la kumzuia mchezaji mmoja,” alisema.
Kocha huyo alisema baada ya kupata mbinu hizo sasa anahitaji kuhakikisha timu yake inapata ushindi katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Uwanja wa Uhuru kesho.
“Mtibwa ni timu nzuri hivyo nimejipanga kuhakikisha kikosi changu kinaingia uwanjani kwa kupata pointi zote tatu muhimu kwa ajili ya kufikia malengo yetu ya kuhakikisha Simba inatwaa ubingwa,” alisema Omog.
Post a Comment