KLABU ya Simba ya Dar es Salaam, imeamua kutumia pesa ili kuhakikisha ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unatua Msimbazi kwa mara ya kwanza baada ya miaka zaidi ya minne.
Hii imekuja baada ya vigogo wa klabu hiyo kuwa tayari kutumia zaidi ya shilingi milioni 300 za Kitanzania kwa ajili ya bonasi na kuwapa motisha wachezaji wao ili kufanikisha kampeni yao ya kuurudisha ubingwa wa Bara Msimbazi.
Ishu nzima iko hivi:- Mabosi na matajiri wanaoikubali Simba wamekubaliana kuchangishana na kutoa shilingi milioni 10 kwa wachezaji kila timu yao inapoibuka na ushindi kwenye mechi zake za kimashindano hasa hizi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Vigogo hao wanaamini kwa kuwapa wachezaji kiasi cha shilingi milioni 10 katika kila mechi wanayoshinda kitaongeza hamasa ya ushindi ndani ya kikosi hicho na mwisho wa msimu ubingwa utatua Msimbazi.
Katika mechi nne ambazo Simba imecheza hadi sasa tayari wachezaji wameshalamba shilingi milioni 30 ambazo zinatokana na ushindi wa mechi zao tatu kati ya nne walizocheza, huku wakikosi milioni 10 katika mechi dhidi ya JKT Ruvu kutokana na kuambulia suluhu ya 0-0.
Hii inamaanisha kuwa katika mechi 30 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu vigogo hao walikuwa wamejipanga kutumia shilingi milioni 300 kama motisha kwa wachezaji wao.



Lakini ukijumlisha na mechi za Kombe la Shirikisho kuna uwezekano dau likawa kubwa zaidi iwapo timu hiyo itafanya vizuri kwenye mechi zake za mashindano hayo ambayo bingwa wake anaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Fedha hizo zinatolewa na kundi moja la wanachama wa Simba ambao huchangishana shilingi milioni 5 katika kila mechi na milioni 5 nyingine inatolewa na bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo’ ambaye aliahidi kutoa kiasi sawa na wanachochangishana wanachama hao.

Mbali na fedha hizo za bonasi, lakini Simba pia imepania kuhakikisha wachezaji wake wote wenye nidhamu na wanaojitoa kwa moyo wao wote kuipigania klabu hiyo hawapandi tena daladala wala bodaboda.
Hii imekuja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Zacharia Hanspope, kujipanga kutoa zawadi ya gari kwa wachezaji wote wenye moyo na wanaojitoa kuipigania timu hiyo kwenye kipindi cha shida na raha.

Katika kufanikisha hilo, tayari Pope ameshamkabidhi zawadi ya gari aina ya Raum na fedha taslimu shilingi milioni 1, beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kutokana na uwezo mkubwa ambao amekuwa akiuonyesha katika kikosi cha miamba hiyo ya Msimbazi.
Baada ya kumkabidhi gari Tshabalala, Pope amedai kuwa huu ni mwanzo tu na ataendelea na utamaduni huu wa kutoa magari kama motisha kwa wachezaji wote ambao watajituma na kujitoa kwa ajili ya timu hiyo.

Post a Comment

 
Top