VITA kali katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya ufungaji bora msimu huu inaonekana kunoga zaidi kufuatia kuwepo kwa ushindani wa hali ya juu kwa mastraika wawili raia wa Burundi, Laudit Mavugo anayekipiga katika klabu ya Simba na Amiss Tambwe, anayechezea Yanga.
Msimu uliopita Tambwe wa Yanga ndiye aliyeibuka mfungaji bora, akifunga mabao 21, lakini msimu huu itabidi jasho limtoke kisawasawa, kutokana na uwezo unaoonyeshwa na Laudit Mavugo wa Simba.
Mpaka sasa Mavugo amefanikiwa kupachika mabao matatu, akiongoza, ambapo alianza kufunga katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Ndanda FC, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, akafunga tena dhidi ya Ruvu Shooting kwenye ushindi wa mabao 2-1, na kuhitimisha kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kwa upande wa Tambwe, hakufanikiwa kufunga bao lolote katika mchezo dhidi ya African Lyon, Wanajangwani hao wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0, akashindwa pia kufunga walipotoa suluhu ya 0-0 na Ndanda FC, akaja kuzinduka dhidi ya Majimaji, akifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0.


Mavugo anahitaji kuweka rekodi ya kuibuka mfungaji bora kama alivyokuwa akifanya katika Ligi ya Burundi, kwani msimu uliopita alifunga mabao 32 na sasa anataka kufanya hivyo Ligi ya Tanzania, huku Tambwe naye akitaka kumzidi ujanja.
Mashabiki wa Simba wanampa nafasi kubwa Mavugo kuibuka mfungaji bora, kitu ambacho kinamuudhi Tambwe, ambaye naye ameamua kuweka wazi kuwa atawafunga midomo.
“Mabao niliyofunga katika mchezo dhidi ya Majimaji ni sawa na kupasha msuli moto kwa ajili ya kuisubiri Simba, nitahakikisha naifunga kwa mara ya tatu,” alisema.
Kwa upande wake, Mavugo alisema: “Ni kweli nahitaji kuendelea na ufungaji bora, suala hilo liko pale pale, kwani malengo yangu ni kuhitaji kufunga mabao mengi na kuvunja rekodi ya mshambuliaji bora wa msimu uliopita,” alisema.


Post a Comment

 
Top