UONGOZI wa klabu ya Majimaji umempa
mkataba wa mwaka mmoja aliyekuwa kocha wao wa msimu uliopita, Kalimangonga
Ongala, kwa ajili ya kuendelea kuinoa timu hiyo Ligi Kuu Tanzania Bara.
Awali, Ongala alikuwa akiinoa timu
hiyo na kufanikiwa kuibakisha kwenye Ligi Kuu ambapo msimu huu ulipoanza aligoma kuendelea nayo kutokana na ukata
lakini sasa ameamua kurejea.
Umuhimu wa Kali umeonekana wazi kwani
katika michezo sita ambayo wamekwisha kucheza mpaka sasa hawajapata matokeo
mazuri kwani wamefungwa yote wakiburuza mkia kwenye msimamo wa ligi.
Akizungumza jana mwenyekiti wa timu
hiyo, Humphrey Milanzi, alisema tayari wamemalizana na Ongala hivyo ameanza
kazi rasmi.
“Tumempa mkataba wa mwaka mmoja
Jumatatu na leo (jana) aliwasili Songea mchana kwa ndege akitokea Dar es Salaam
na kuungana na timu moja kwa moja kuendelea na maandalizi ya mchezo ujao,”
alisema.
Alisema kwa sasa wanaendelea kujiwinda
na mchezo wao dhidi ya Stand United unaotarajia kuchezwa Jumapili kwenye uwanja
wao wa nyumbani wa Majimaji.
Post a Comment