KUNA uwezekano mkubwa wadau mbalimbali wa soka walijiuliza sababu ya kukataliwa kwa penalti mbili za Simon Msuva, katika mchezo wa juzi dhidi ya Majimaji ambao Yanga walishinda kwa mabao 3-0.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na mwamuzi Emanuel Mwandembwe kutoka Arusha, akisaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga pamoja na Silvestre Mwanga kutoka Kilimanjaro, liliibuka tukio la utata baada ya Msuva kulazimika kurudia kupiga penalti mara tatu.
Picha kamili lilikuwa hivi: Yanga walipata penalti dakika ya 15, baada ya mchezaji wa Majimaji, Ernest Raphel kuunawa mpira kwenye eneo la hatari na hivyo mwamuzi Mwandembwe kuamuru ipigwe penalti.
Msuva ndiye aliteuliwa na Yanga kupiga penalti hiyo, lakini penalti zake mbili za mwanzo licha ya kufunga mwamuzi alimuamuru arudie hadi kwenye ile ya tatu ambayo iligonga mwamba na Deus Kaseke kumalizia.

Kutokana na kuibuka na maswali ya kwa nini Msuva alitakiwa kurudia zaidi ya mara moja penalti yake, BINGWA limekwenda mbali zaidi kwa kumtafuta mmoja wa waamuzi wa soka Tanzania mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ili kujua kanuni zinasemaji.
Mwamuzi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa sababu sheria zinambana kuzungumzia soka wakati akiwa bado anachezesha, alisema kuwa mwenzake alitumia sheria ya 14 kwenye mchezo wa soka katika kufanya maamuzi.
Alisema kuwa sheria hiyo namba 14 ina vipengele vingi na ndiyo inazungumzia pigo la penalti, huku akifafanua kuwa kama pigo la penalti linapigwa kabla mpigaji hajapiga beki na ndugu yake na anayepiga penalti wakaingia ndani ya 18, basi pigo linarudiwa hata kama mpiga anakosa au kupata bao lazima pigo litarudiwa.
“Iwapo kama timu A wanapiga penalti lakini kabla haijapigwa wachezaji wa timu A na B wakiingia  kabla basi pigo litarudiwa hata kama mpigaji wa timu A amekosa au amepata, ”alisema.
Mbali na maelezo hayo, BINGWA liliitafuta sheria hiyo ambayo inaelezea kwa kina zaidi upigaji wa penalti katika dakika 90 za mchezo au zile tano tano za mwisho.
Sheria hiyo inasema, wachezaji wote wanatakiwa kuwa nje ya 18, isipokuwa mwamuzi wa kati na golikipa naye kuwa langoni, iwapo kama itatokea wasiostahili kuwa ndani ya 18 wakaingia kwa namna yoyote penalti hiyo inapaswa kurudiwa.
Mipigo yote inatakiwa kupigwa kutokea katika alama ya kupigia penati, huku golini kukiwa na golikipa wa timu tofauti na mpigaji.
Kipa anatakiwa kubaki katikati ya milingoti miwili huku akiwa amesimama katika mstari wa goli mpaka pale mpira utakapokuwa umepigwa, ingawa anaweza kurukaruka, kunyoosha mikono, kwenda upande mmoja mpaka mwingine akiwa ndani ya mstari wa goli.
Hakuna mchezaji wa timu ya mpigaji anaruhusiwa kuugusa mpira.
Mpira unaweza kumgusa golikipa, milingoti ya pembeni na wa juu kwa idadi yoyote na kurudi uwanjani kisha mchezaji mwingine aliye kwenye nafasi nzuri akafanikiwa kuweka nyavuni na hilo linahesabika ni bao.
Iwapo kama penalti inapigwa kabla ya mwamuzi wa kati au wa pembeni waliopo karibu na goli kupiga kipenga kuashiria goli, wachezaji wakaonekana kuingia ndani ya 18 penalti inatakiwa kurudiwa.

Post a Comment

 
Top