AMA kweli Masau Bwire hakosi la kusema hata
kama akifungwa! Safari hii ameibuka na jipya baada ya awali kumbeza straika wa
Simba, Laudit Mavugo ambaye alisema mashabiki watamuita straika huyo kinyozi
kwani hataweza kufanya lolote dhidi yao.
Kabla ya mchezo wa Simba dhidi ya Ruvu
Shooting uliopigwa juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar, Bwire ambaye ni
Ofisa Habari wa Ruvu, alitamba vijana wake watamdhibiti Mavugo kiasi kwamba
atakosa la kufanya, lakini haikuwa hivyo kwani ndiye aliyefunga bao la pili kwa
Simba kwenye ushindi wa mabao 2-1.
Baada ya mchezo huo, Bwire alisema: “Unajua
Watanzania wengi wanampaisha sana Mavugo wakati ni mchezaji wa kawaida tena
sana.
“Kiwango chake si cha kutisha na hata mabao
yake anayoyafunga ni ya kawaida, kama leo (juzi) bao lake ni la bahati, mabeki
wetu walijichanganya kidogo wakamuacha peke yake ndiyo akafunga.
“Ninao vijana wa darasa la nne nawafundisha
soka, kila siku nawaona wanafunga mabao kama yale ya Mavugo kwani ni rahisi mno
na sidhani kama kuna mtu anaweza kukosa akiwa eneo lile.”
Tayari Mavugo ameshafunga mabao mawili msimu
huu baada ya kucheza michezo mitatu akiwa na Simba. Bao lake la kwanza kufunga
ilikuwa kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Ndanda wakati Simba iliposhinda mabao
3-1.



Post a Comment