JOTO la pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga limeanza
kupanda, baada ya kocha wa Wekundu wa Msimbazi, Joseph Omog, kusema tayari
amesoma mbinu za wapinzani wao.
Wakongwe hao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
wanatarajia kukutana Oktoba Mosi, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar
es Salaam.
Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Omog akiwa na Simba dhidi
ya Yanga, baada ya kujiunga na timu hiyo katika msimu huu, lakini akiwa anaijua
vizuri Yanga kabla, ambayo alikutana nayo mara tatu akiwa kocha wa Azam FC.
Ili kuhakikisha anafuta uteja kwa Yanga, Omog alisema
ameendelea kukijenga kikosi chake ili kiweze kupata ushindi katika kila mechi ya ligi hiyo, ikiwemo ya watani wao wa jadi.
“Siangalii mechi ya
Yanga pekee, lakini kimsingi kama wapinzani wetu nawafuatilia na nawasoma
wanavyocheza, kwa kweli ni wazuri, wana hesabu nzuri sana ambazo nazifanyia
kazi kuzizima siku hiyo,” alisema Omog.
Katika hatua nyingine, kocha msaidizi wa timu hiyo, Jackson
Mayanja, wamewaangalia Yanga na kuibuka na kauli moja kwamba wao wataendelea
kusonga mbele baada ya kuifunga bao 1-0 Azam.
Simba walichomoza na ushindi huo katika mechi iliyochezwa
juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, uliowawezesha kukwea
kileleni kutokana na pointi 13, wakifuatiwa na Yanga na Azam, ambao wana pointi
10, lakini wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Mayanja alisema alifurahi kupata ushindi huo ambao ni muhimu
kwa timu yake, kwani malengo yao ni kurejesha heshima ya Msimbazi iliyopotea
kwa miaka kadhaa kwa kushindwa kuchukua taji la ligi hiyo.
Alisema baada ya
kukalia usukani wa ligi hiyo hawatarajii kuteremka kutokana na ubora wa
kikosi chao msimu huu.
“Tunashukuru kwa ushindi
huu tuliopata, maana tulicheza na timu nzuri na tulihitaji kushinda ili
tutimize malengo yetu ya kukaa kileleni,
hatufikirii kushuka tena,” alisema Mayanja.
Wachezaji wa timu hiyo wamepewa siku mbili za mapumziko,
ambapo kesho wataanza mazoezi kujiandaa
na mechi itakayofuata dhidi ya Majimaji, itakayochezwa Septemba 24, mwaka huu, kwenye Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam.
Post a Comment