SIMBA wanajua kuwa wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 10, sawa na Azam FC inayoongoza, sasa Wekundu hao wa Msimbazi wamekoki bunduki zao kuhakikisha Wanalambalamba hao wanakufa kifo kibaya mwishoni mwa wiki hii.
Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa wageni wa Azam FC Jumamosi ijayo katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, ambapo timu itakayoibuka na ushindi itapaa katika kilele cha msimamo wa ligi hiyo.
Kutokana na ugumu wa mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, aliamua kuacha kwenda Uwanja wa Uhuru mwishoni mwa wiki iliyopita kuangalia mchezo kati ya Yanga na Majimaji, na badala yake akajifungia chumbani kuangalia Luninga ili kuisoma Azam FC, iliyokuwa ikikabiliana na Mbeya City katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya.
Katika mchezo huo, Omog alishuhudia Wanalambalamba hao wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1, ambapo inaonyesha dhahiri amefanikiwa kusoma mbinu zao kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi.

Omog, tangu aanze kuinoa Simba, itakuwa ni mara yake ya kwanza kukutana na timu yake ya zamani ambayo aliwahi kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/13, hivyo atataka kuwaonyesha kuwa walimtimua kwa makosa na sasa amerudi akiwa na vitu adimu kwa timu yake hiyo mpya.
Hata hivyo, Omog aliiambia Dimba kwamba licha ya kuzijua timu zote hizo mbili, lakini kamwe hatowadharau wapinzani wake kwa vile anafahamu nia ya kila timu ni kushinda ili iweze kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi hiyo.
“Najua mchezo utakuwa mgumu, kwani sasa kila timu itahitaji kushinda ili iongoze ligi, hali hii inaufanya mchezo kuwa mgumu sana,” alisema.
Akiwa Azam, Omog aliwahi kukutana na Simba katika misimu miwili tofauti ambapo 2013/14 , Simba walipoteza michezo yote miwili, wakifungwa mabao 2-1 mzunguko wa kwanza na ushindi kama huo mzunguko wa pili.
Msimu uliofuata wa 2014/15, Omog akiwa katika benchi la Azam aliendeleza rekodi yake nzuri mbele ya Simba, ambapo mchezo wa mzunguko wa kwanza walitoka sare ya kufungana bao1-1 na mchezo wa mzunguko wa pili Wanalambalamba hao wakashinda 2-1.

Katika hatua nyingine, kwa kile kinachoonekana kumtishia kipa wa Azam FC, Aishi Manula, Straika wa Simba, Laudit Mavugo, amesema atahakikisha anamfunga ili kuipa timu yake ushindi na kukaa kileleni.
Mavugo alisema: “Kilichopo mbele yangu ni kuhakikisha ninaisaidia timu kushinda mchezo huo, naamini kwa kushirikiana na wenzangu tutashinda, ila nitafurahi zaidi kama nitafunga bao, najipanga kufanya hivyo,” alisema.

Post a Comment

 
Top