MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Klabu ya Yanga, imeamua kuja na staili ya ‘biashara asubuhi jioni mahesabu’, baada ya kuanza mchakato wa usajili mapema ili dirisha la usajili likifunguliwa tu waimarishe kikosi chao.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo BINGWA linazo, Yanga ambayo kwa siku za karibuni imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kiungo namba sita, tayari imeanza kusaka mafundi wa kuimarisha eneo hilo ili kuwaweka vizuri zaidi msimu huu.
Kutokana na hali hiyo, tayari kamati ya mashindano chini ya Mwenyekiti wake, Mhandisi Paul Malume, aliyevaa viatu vya Isaac Chanji, aliyejiudhulu hivi karibuni ilikutana na Mwenyekiti wa klabu hiyo na kuanza mikakati ya kufanya usajili kuelekea dirisha dogo litakalofunguli Desemba 15, mwaka huu.
BINGWA lina taarifa kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanasakwa na Yanga ni pamoja na straika wa kimataifa wa Zimbabwe, Walter Musona, ambaye alikuwa chaguo la kwanza la Hans van der Pluijm, kabla ya ujio wa Mzambia Obrey Chirwa.
Mbali na staa huyo, pia yupo kiungo wa chini wa klabu ya APR ya Rwanda, Bizimana Djihad, ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji walioisumbua sana Yanga wakati timu hizo zilipokutana kwenye hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwaka huu.
Benchi la ufundi la Yanga linaamini kuwa Djihad ataweza kumaliza tatizo la kiungo mkabaji ambalo halijawahi kupata suluhu kwenye kikosi cha miamba hiyo ya Jangwani tangu alipoondoka Athuman Iddi ‘Chuji’.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya Yanga, kinadai kuwa Kocha Hans van der Pluijm ameshaweka wazi kuwa kwa Tanzania hakuna kiungo mkabaji ambaye ana vigezo anavyovitaka.
“Baada ya kocha kuona hakuna mchezaji wa kucheza namba sita, huku kukiwa kuna tatizo kubwa nafasi hiyo, tulimpa nafasi ya kupendekeza, ndipo jina la Djihad lilipojitokeza, nasi tupo kwenye mpango wa kuanza kuangalia iwapo kama upo uwezekano wa kumpata kwenye usajili wa dirisha dogo au la,” alisema.
Mtoa habari wetu ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kuwa kama mkataba wa Musona ukimalizika Desemba mwaka huu, klabu itamfuata.
“Musona alikuwa chaguo letu la kwanza kabla ya kumsajili Chirwa, lakini klabu yake ilimbana tukashindwa kumsajili, lakini safari hii kama mkataba wake ukiisha hiyo Desemba na akawa huru tutakwenda kumsajili kama kawaida,” alisema.
Alisema kama wachezaji hao wawili watapatikana wataangalia, kuna uwezekano mkubwa sana wachezaji wawili wa kimataifa wakatemwa kupisha mastaa hao, au wakaongezwa kama sheria ya wachezaji 10 wa kigeni ikipitishwa.
Akizungumzia uwezekano wa Mrisho Ngassa na Mbrazil Andrey Coutinho kusajiliwa Yanga, mtoa habari wetu aliliambia BINGWA kuwa uwezekano wa wawili hao kurudishwa Jangwani unategemea zaidi kauli ya kocha.
“Coutinho yupo, lakini si kwa mwaliko wetu, yupo kwa mdau mkubwa Yanga, Musebene, hivyo kama kocha ataona anamfaa tutampa nafasi, kikubwa tunataka kuona Yanga inakuwa tishio katika mashindano ya ndani na ya nje.
“Kuhusu suala la Ngassa, juzi tumekaa kwenye kikao pamoja na mwenyekiti wetu, lakini mpaka tunamaliza suala la Ngassa halikujadiliwa, ingawa tuna taarifa kuwa alishakutana na Mwenyekiti na kuzungumza,” alisema.
Post a Comment