BEKI wa Yanga, Pato Ngonyani,  amewaangalia washambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo na kujiridhisha ataweza kuwazuia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itakayochezwa Oktoba mosi, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ngonyani, ambaye  hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, alisema  akipanga atawaonyesha kazi wawili hao.

Ngonyani alisema yuko fiti, baada ya kupona majeraha ya muda yaliyosababisha kuwekwa benchi na kocha wake.
Alisema akipewa nafasi ya kucheza, atahakikisha anawashangaza mashabiki wengi, kwani itakuwa ni vigumu kupitwa na washambuliaji wa Simba.
“Nipo tayari kucheza, sina wasiwasi hata kidogo, ingawa ni mchezo ambao unavuta hisia za maelfu ya mashabiki, lakini kwangu mimi ni kawaida,” alisema Ngonyani.
Msimu uliopita, Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

 
Top