KWANINI Yanga inamhofia Ajib? Hili ndilo swali ambalo mashabiki wa Simba wanajiuliza kwa sasa baada ya kuwa na tetesi kuwa inaandaliwa mikakati ya kuhakikisha straika huyo anakosa baadhi ya mechi za Wanamsimbazi hao.
Picha kamili liko hivi:- Ajib ana kadi mbili za njano na iwapo akipata kadi ya tatu basi atakosa mechi moja ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kitu ambacho ni pigo kwa Wekundu hao wa Msimbazi kutokana na kiwango alichokionyesha straika huyo hadi sasa kwenye VPL.
Simba inatarajiwa kuivaa Azam keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru.
Lakini wakati Ajib akiwa na kadi hizo mbili za njano baadhi ya mashabiki na wanachama wenye majina makubwa wa Simba wameshausoma mchezo na sasa wanahofia kuwa staa wao huyo anaweza kutengenezewa mazingira ya kupata kadi nyingine ya njano ili akose mechi moja.
Kinachowatesa zaidi mashabiki hao ni hofu kuwa mechi dhidi ya Yanga haiko mbali sana wanadhani kunaweza kuwa na hujuma ya kumtengenezea Ajib kadi nyingine ya njano kwenye mechi moja kabla ya ile ya Oktoba mosi ili akose Kariakoo Dabi.
“Ajib ana kadi mbili za njano na kama akipata kadi ya tatu atakosa mechi moja,” alisema mdau mmoja wa Simba. “Lakini, tatizo mechi ya Yanga ipo karibu sana na kuna tetesi kuwa anaweza kutengenezewa kadi mechi moja kabla ya kuwavaa Yanga ili asiwepo uwanjani Oktoba mosi.
“Yaani kwa kifupi sijui kwanini hawa Yanga wanamwogopa sana Ajib mpaka wamwandalie zengwe hili cha msingi tuwe makini na tumlinde tu.”
Mbali na vigogo hao kuapa kumlinda straika huyo, pia kocha wake, Joseph Omog, ameandaa mikakati mipya ya kumlinda na mabeki wa timu pinzani wanaokuwa wanamkamia.
Kocha huyo wa zamani wa Azam, amegundua hilo na kulifanyia kazi ambapo anaamini kwamba mabeki wa timu pinzani wamekuwa wakiwakaba sana mastraika wao, Ajib na Laudit Mavugo.
“Ninaendelea kuwanoa washambuliaji wangu wote pamoja na viungo kwa kuwapa saa kwa ajili ya kutengeneza umakini pamoja na mbinu za mabeki ambao wanakuja kwa lengo la kumzuia mchezaji mmoja,” alisema Omog.
Post a Comment