MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga leo wameichapa
Majimaji FC ya kutoka Songea kwa mabao 3-0 katika mchezo wa ligi uliopigwa
Uwanja wa Uhuru jijini Dar.
Yanga ambayo kabla ya kuvaana na Majimaji leo ilikuwa
imeshuka uwanjani mara mbili, mechi ya kwanza wakipata ushindi wa mabao 3-0
dhidi ya African Lyon wafungaji wakiwa ni Juma Mahadhi, Deus Kaseke na Simon
Msuva, mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Baada ya hapo vijana hao wa Jangwani walisafiri hadi mkoani
Mtwara kucheza na Ndanda katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona lakini mchezo huo
uliisha kwa suluhu.
Katika mchezo wa leo uliopigwa Dimba la Uhuru, Yanga
ikishuhudiwa na kiungo wake wa zamani, Mbrazil Andrey Coutinho iliuanza mchezo
huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa Deus Kaseke bao
ambalo lilidumu kipindi cha kwanza chote.
Kipindi cha pili Yanga walirudi kasi na kutengeneza nafasi
nyingi za mabao lakini washambuliaji hawakuwa makini kuzimalizia. Alikuwa ni
Amissi Tambwe aliyefanikiwa kuwainua mashabiki wa timu hiyo baada ya kufunga
bao kwa shuti dakika ya 79 akiunganisha krosi ya Juma Mahadhi ambaye aliingia
kipindi cha pili badala ya Obrey Chirwa.
Alikuwa ni Tambwe tena ambaye msimu uliopita alikuwa
mfungaji bora kwenye VPL akitupia kambani mabao 21, ambapo alifanikiwa kurejea
kambani tena na kufunga bao la tatu na kuipa uhakika wa pointi tatu timu yake
ya Yanga.
Yanga sasa imefikisha alama saba baada ya kushuka uwanjani
mara tatu, kati ya hizo imeshinda mbili na sare moja huku Majimaji ikibaki
mkiani ikiwa haina pointi kutokana na kupoteza michezo yote minne iliyocheza
mpaka sasa.
Post a Comment