WAKATI Yanga ikishuka dimbani leo kuivaa Mwadui ya mkoani Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, klabu hiyo imetakiwa kufanya kila linalowezekana kumsajili kiungo mkabaji mahiri, Jonas Mkude wa Simba, kama inataka kuwa bora zaidi na hatimaye kutetea ubingwa wao huo, ikiwamo kutamba kimataifa.
Mbali ya Mkude, viungo wengine wanaotajwa kuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga kwa hapa nchini, ni Mudathiri Yahya na Himid Mao, wote wa Azam.
Kati ya wachezaji hao, ambaye anastahili kumpisha mmoja wa viungo hao, ni Mbuyu Twite, ambaye amekuwa akitumiwa na Yanga kama kiungo mkabaji, beki namba mbili, beki wa kati na wakati mwingine akipangwa kushoto pale ilipohitajika kufanya hivyo.
Lakini kwa wakati huu ambao Twite ambaye asili yake ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akiwa na uraia wa Rwanda, ameonekana kupoteza makali yake, ikielezwa hilo limetokana na umri kumtupa mkono, huku pia akiwa si fundi wa kuitumikia ipasavyo nafasi ya kiungo mkabaji.
Kwa muda mrefu, wapenzi wa Yanga wamekuwa katika kilio cha kusaka kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kukaba, kupambana kulingana na aina ya mchezo na kupandisha timu pale ilipohitajika.
Tangu kuondoka kwa kizazi cha wachezaji kama Method Mogela ‘Fundi’, Athumai Idd ‘Chuji’, Frank Domayo, Juma Seif ‘Kijiko’ na wengineo wa aina yao, Wanajangwani hao wameshindwa kupata warithi sahihi wa wakali hao.
Kutokana na hilo, huenda neema ya kuvaa uzi wa Jangwani ikawaangukia mmoja wao kati ya Mkude, Mudathir na Mao, ambao wanatajwa kuwa suluhisho la tatizo hilo kwa mabingwa hao wa soka hapa nchini.
Mbali ya Twite, wachezaji ambao wamekuwa wakitumika kama viungo wakabaji Yanga ni Pato Ngonyani, Said Juma Makapu na Vincent Andrew ‘Dante’, ambao wameshindwa kukidhi mahitaji ya Kocha Hans van der Pluijm, kiasi cha wakati mwingine kumpanga Thaban Kamusoko, ambaye hucheza vizuri zaidi akipangwa kama kiungo mshambuliaji.
Kwa kuona hilo, tayari matajiri wa Yanga wameamua kwenda mafichoni kwa ajili ya kusaka saini ya mmoja kati ya nyota wanaoweza kuwa suluhisho la tatizo lao, huku Mkude akiwa ndiye anayetolewa macho zaidi, akifuatiwa na Mudathir.
Katika kupigilia msumari juu ya mkakati huo wa Yanga, mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Ali Mayay, amewashauri vigogo hao akiwataka kufanya kila linalowezekana kumsajili mmoja wa viungo hao watatu, akiamini ndio wenye uwezo wa kuimarisha safu ya kiungo cha klabu hiyo ya Jangwani.
“Hao viungo watatu wana sifa zote anazozitaka Pluijm na endapo timu hiyo itataka kuwasajili, ni lazima wavunje benki.
“Wana uwezo wa kucheza soka la aina yoyote, lakini pia wana uzoefu na michuano ya kimataifa, kwani wote watatu wameweza kuitumikia Taifa Stars katika nyakati tofauti,” alisema Mayay.
Mayay aliongeza: “Hata kiumri, viungo hao bado umri wao unawaruhusu kucheza soka ya kasi, kukaba kwa nguvu na kupambana katika hali yoyote tofauti na akina Kamusoko na Twite.”
Mayay alikwenda mbali zaidi na kusema endapo Yanga watafeli kuwasajili wachezaji hao, itawalazimu kuvuka mipaka kusaka kiungo mkabaji ambaye atakuwa na sifa kama za akina Mkude.
Tayari kuna tetesi kuwa matajiri wa Yanga wapo katika mkakati kabambe wa kutatua tatizo hilo sugu la kiungo mkabaji, huku ikielezwa kuwa Mkude yupo katika mkakati wa kutimkia Afrika Kusini, baada ya kumalizika kwa mkataba wake ndani ya Simba.
Habari zaidi zinadai kuwa safari hiyo ya Mkude ya kwenda Afrika Kusini ni moja ya janja ya kiungo huyo kutaka kumalizia safari yake katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa Simba unaonekana kushtukia dili, hivyo kujipanga kumdhibiti kiungo wao huyo kwa kumpa mkataba mnono pamoja na gari kama walivyofanya mapema wiki hii kwa beki wao wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Kwa upande wa Mudathir na Mao, klabu yao ya Azam huwa haina shida katika suala lolote la kuuza wachezaji ambapo klabu yoyote yenye uwezo wa kufikia dau, huwa huru kumsajili nyota yeyote kutoka kwa Wanalambalamba hao wa Mbagala Chamazi, jijini Dar es Salaam.
Juu ya mchezo wao wa leo, Yanga kupitia kwa kocha wao, Pluijm, wametamba kushinda na kuzidi kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao.

Post a Comment

 
Top