STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe
anaonekana si lolote baada ya kushindwa kufunga katika mechi mbili za timu yake
katika Ligi Kuu Bara, lakini amesikia kejeli hizo na kusema: “Mnaleta dharau?
Tukutane Oktoba.”
Tambwe msimu uliopita alitwaa Tuzo ya
Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 21, lakini sasa mambo
magumu na katika mchezo uliopita wa Yanga dhidi ya Ndanda FC alitumika kama
kiungo mshambuliaji badala ya mshambuliaji kamili.
Kinachomfanya Tambwe abezwe na
mashabiki hasa wa Simba ni kitendo cha washambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib,
Laudit Mavugo na Frederic Blagnon wote kufunga bao katika mechi tatu za ligi
kuu.
Mavugo, raia wa Burundi, kama ilivyo
kwa Tambwe ana mabao mawili, Blagnon wa Ivory Coast na Ajib wamefunga bao moja kila
mmoja sawa na Shiza Kichuya. Hao wameifungia Simba jumla ya mabao matano.
Yanga ina mabao matatu katika mechi
mbili na Tambwe amesema kuwa, anasikia na kuona jinsi anavyodharauliwa na
mashabiki wa Simba lakini amewataka kusubiri atakapokutana nao.
“Habari zao nishazipata,we waache tu
waendelee kunidharau ila tutakutana uwanjani Oktoba (Mosi) kwani dawa yao
ninayo na wao wanalijua hilo, pia wanatambua huwa sitabiriki.
“Msimu uliopita nimewafunga mara
mbili, hata Ajibanajua hilo ila napenda kumshauri kuwa kama anataka msimu huu
kuwa mfungaji bora ni jambo zuri na anatakiwa kuongeza bidii.
“Kila straika anataka kuwa mfungaji
bora, hata mimi nataka kuwa mfungaji bora tena,” alisema Tambwe ambaye leo
anaweza kuichezea Yanga dhidi ya Majimaji ya Songea katika mchezo wa ligi kuu
kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kinachomfanya Tambwe atambe ni kwamba,
katika msimu uliopita wa ligi kuu aliifunga Simba katika mechi mbili ya
nyumbani na ugenini yaani Septemba 26, mwaka jana na Februari 20, mwaka huu.
Mara zote Yanga ilishinda mabao 2-0.
Yanga na Simba zitakutana Oktoba Mosi,
mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika muendelezo wa ligi kuu.
Post a Comment