SIMBA wanatarajia kuwakosa wachezaji wawili tegemeo, kiungo  Mwinyi Kazimoto na beki wa kati, Method Mwanjale, katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Majimaji, itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mwanjale alipata mchubuko wa nyama katika paja kwenye mechi iliyopita dhidi ya Azam, iliyochezwa Uwanja wa Uhuru na wao kushinda bao 1-0.
Mwinyi atakosa mechi ya pili  baada ya kuumia goti katika mechi ya Mtibwa Sugar  iliyochezwa Septemba 11, mwaka huu,  kwenye Uwanja wa Uhuru na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alisema  anatarajia kuwakosha wawili hao katika kikosi chake kitakachocheza na Majimaji kutokana na kuwa majeruhi.
Omog alisema anatarajia kuwatumia wachezaji wengine kuziba nafasi zao, kwani malengo yake ni kuibuka na ushindi ili kuendelea kuongoza katika msimamo wa ligi hiyo.
 Alisema kikosi chake kina wachezaji wengi ambao anaweza kuwatumia katika mechi hiyo, ambayo ni muhimu kwake kupata pointi tatu.
Omog alisema pamoja na mechi hiyo haitakuwa rahisi kwao kushinda, lakini itakuwa ni kipimo kizuri kuendea pambano lao la watani wa jadi Yanga litakalochezwa Oktoba mosi, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Alisema anaendelea kukiboresha kikosi chake katika mazoezi yanayoendelea kwenye Uwanja wa Boko Veterani ili  kukijengea ufiti zaidi.

Post a Comment

 
Top