WAKATI  joto la pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga likizidi kupanda, winga machachari wa Simba, Jamal Mnyate, ametibua nyongo ya kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, kutokana na kushindwa kuelewa maelekezo  yake katika mazoezi yaliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Boko Veterani,  jijini Dar es Salaam.
Simba walifanya mazoezi hayo kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Majimaji, utakaochezwa kesho, lakini wakielekeza nguvu katika pambano lao na Yanga litakalochezwa  Oktoba mosi, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa.
Katika mazoezi hayo, Omog alionekana kuwanoa viungo  kupiga krosi safi  na washambuliaji kuweza kufunga ,  lakini mabeki wa pembeni kupanda na mpira  kusaidia mashambulizi.
Mnyate alionekana kushindwa kufuata maelekezo ya Omog, kwani kila mara alikwenda kinyume na kile alichohitaji kocha huyo katika mazoezi hayo.
Katika zoezi hilo lilichukua dakika 15, kiungo wa timu hiyo, Jonas Mkude,  alikuwa anamwanzishia mpira Mnyate na Omog kutaka kuurudisha kwa Mkude kabla ya kupiga krosi.
Zoezi hilo lilionekana gumu kwa Mnyate, kutokana na kutaka kwenda na mpira moja kwa moja na kupiga krosi, kitu ambacho kilionekana kumkera Omog.
 Baada ya kushindwa  kile alichohitaji Omog, Mnyate aliomba msaada kwa Mkude ili aweze kumsaidia kuwa kocha alikuwa anahitaji nini zaidi kutoka kwake.
“Mkude niulizie kwa mwalimu nipite mimi kupiga krosi au Hamad?  Wewe fanya hivyo hivyo…”
Hata hivyo, Omog alilazimika  kwenda kumweleza kwa vitendo baada ya kuona  kwamba alichokuwa anahitaji kwa winga huyo kushindwa.
Simba wanaongoza katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na pointi 13, wakifuatiwa na Yanga na Azam wenye pointi 10, lakini wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku Majimaji wakishika mkia ambao hawana pointi baada ya kufungwa michezo mitano mfululizo.

Post a Comment

 
Top