KOCHA Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans van de Pluijm, hajafurahishwa kabisa na suluhu ya 0-0 waliyoipata dhidi ya Ndanda FC mchezo uliopita na sasa balaa lote litawaangukia Majimaji leo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Yanga iliwakosa baadhi ya wachezaji wake muhimu wa kikosi cha kwanza ambapo sasa jambo la kufurahisha kwa mashabiki wa Wanajangwani hao ni kwamba, bunduki zote zipo kamili.
Kati ya wachezaji waliokosekana kwenye mchezo huo ni kiungo mwenye mambo mengi uwanjani, Haruna Niyonzima ambaye alikuwa kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa ya Rwanda iliyokuwa ikipambania kutafuta kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).
Mbali na Niyonzima, pia Wanajangwani hao walimkosa beki wao ambaye kwa sasa yupo kwenye kiwango cha hali ya juu, Vincent Bossou, ambaye alikuwa akiitumikia timu yake ya Taifa ya Togo, ambapo aliisaidia kutinga katika fainali hizo za Afcon.
Kwa kutambua umuhimu wa mchezo wa leo, Pluijm anatarajiwa kuingiza kikosi kazi ikizingatiwa kuwa kikosi hicho mpaka sasa kinashika nafasi ya saba kwenye msimamo kikiwa na pointi nne kitu ambacho kinawakera sana Wanajangwani hao.
Pointi hizo zinatokana na michezo miwili ambayo wamekwisha kucheza mpaka sasa wakianza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon mabao yakifungwa na Simon Msuva, Juma Mahadhi na Deus Kaseke, huku mchezo wa pili wakitoka suluhu ya 0-0 na Ndanda FC.
Yanga ndiyo timu ambayo imecheza michezo miwili sawa na JKT Ruvu, huku timu nyingine kila moja ikiwa imecheza michezo mitatu hiyo ikimaanisha kuwa Wanajangwani hao wana mchezo mmoja mkononi.
Jambo linalowapa jeuri Yanga kwamba wataibuka na ushindi katika mchezo wa leo ni kwamba wanacho kikosi cha maangamizi kuanzia safu ya ulinzi hadi ushambuliaji, kazi kubwa ikiwa kwa kocha kupanga mwenyewe amwanzishe nani na nani aanzie benchi.
Lingine ambalo linawapa Wanajangwani hao moyo wa kuibuka na ushindi wa mabao mengi ni kwamba Majimaji kwa sasa wanaonekana kutokuwa vizuri kuanzia uchezaji wao na pia inasemekana hata mishahara kwa wachezaji wamekuwa hawapati kwa muda.
UWANJA WA UHURU AMBAO YANGA WATACHEZEA LEO NA MAJIMAJI |
“Sisi tumejipanga kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu ndiyo maana kila mechi tunaichukulia kwa uzito mkubwa, tunajua kwamba hata wenzetu wamejipanga ila kwa kikosi tulichonacho tuna imani kubwa kwamba tutatimiza malengo yetu,” alisema.
Katika mchezo huo matumaini makubwa kwa mashabiki wa Yanga ni kwa washambuliaji wao, Donald Ngoma, Obrey Chirwa pamoja na mfungaji bora wa msimu uliopita Mrundi, Amissi Tamwe.
Timu hizi zilipokutana msimu uliopita Yanga waliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0, mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Post a Comment