PAMOJA na kubeba ubingwa wa Kombe la
Chalenji, wachezaji wa kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara,
Kilimanjaro Queens wamekiona cha mtema kuni baada ya kusotea posho zao kwa
zaidi ya saa tano kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Soka Tanzania (TFF).
Akina dada hao, walibaki kwenye ofisi
za TFF, wakitaka walipwe posho zao dola 160 (Sh 341,000) kila mmoja lakini
ilionekana ni vigumu.
“Kweli bado tuko hapa, tumechoka,” alisema
mmoja wa wachezaji chipukizi wa timu hiyo wakati alipozungumza na gazeti hili
jana saa 8 mchana.
“Tumetoka Airtel kuja hapa, wamesema
watatulipa leo lakini imeshindikana na vibaya zaidi wanatujibu vibaya, kweli
hatujapenda.”
Saa 12 jioni, mchezaji mwingine
alizungumza na gazeti hili na kusema: “Tumeondoka tayari, kila mmoja amelipwa
dola 60 (Sh 128,000), bado dola mia ambayo hatuna uhakika kama tutaipata. Watu
wamechukia sana, unajua tulijituma sana.
“Kule tulipewa posho ya mwanzo tu,
tunaamini hawakuamini tutafika mbali. Mechi zote za mwisho hasa za mtoano,
hatukuwa tumelipwa posho lakini tulipambana sana. Ajabu, bado wanatusumbua.”
Simu za viongozi wa TFF, zilikuwa
hazipokelewi lakini siku chache zilizopita baada ya Kili Queens kutwaa ubingwa,
waliahidiwa dola 11,000 (zaidi ya Sh milioni 23) kutoka kwa Rais wa TFF, Jamal
Malinzi.
Kina dada hao wamepata sifa kubwa
kutokana na kubeba kombe hilo lakini mzunguko huo wa posho, unaweza kuwakatisha
tamaa kupambana wakati mwingine.
Post a Comment